May 09, 2024 07:05 UTC
  • Kuthibitishwa ukweli wa utawala wa Kizayuni kutoweza kujilinda; matokeo muhimu ya vita vya Gaza

Wachambuzi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kujilinda bila ya msaada wa Marekani, na udhaifu wake katika uwanja huo umefichuka na kuanikwa peupe.

Zaidi ya miezi 7 imepita tangu utawala wa Kizayuni uanzishe mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza. Katika kipindi hiki, karibu watu elfu 35 wameuawa shahidi na zaidi ya wengine elfu 76 wamejeruhiwa. Mbali na jinai hiyo dhidi ya watu wa Gaza, lakini vita hivi vimekuwa na athari nyingi kwa utawala wa Kizayuni, baadhi zikiwa ni za kistratijia.

Moja ya matokeo ya kistratijia ya vita hivi ni kuongezeka chuki ya mataifa ya ulimwengu dhidi ya jinai zinazofanywa na utawala kwa watu wasio na hatia, hasa wanawake na watoto. Huku watu wa nchi tofauti wakitangaza uungaji mkono wao kwa Gaza na kuchukizwa kwao na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kufanya maandamano katika pembe tofauti za dunia, wanataaluma wa ulimwengu nao pia wamechukua misimamo ya wazi ya kupinga jinai za utawala huo ghasibu na kuchukizwa kwao na hatua za kichokozi za Tel Aviv.

Katika kivuli cha kutojali na hata uungaji mkono wa madola ya kibeberu duniani hususan Marekani kwa mauaji ya kimbari huko Gaza, wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani na nchi za Ulaya wanaendelea kufanya maandamano makubwa ya kuwatetea watu wa Gaza na kulaani jinai za Wazayuni. Maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani na Ulaya na uungaji mkono wa idadi kubwa ya wahadhiri wa vyuo hivyo kwa maandamano hayo ni dhihirisho madhubuti na la wazi la kuchukizwa wasomi wa kimataifa na utawala wa Kizayuni.

Natija nyingine muhimu ya kistratijia ni kufichuliwa udhaifu wa kijeshi na kijasusi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala huo si tu kwamba ulishinda kutabiri na kuzuia operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa iliyotekelezwa kwa mafanikio na Hamas mnamo tarehe 7 Oktoba, lakini pia katika kipindi cha miezi 7 iliyopita umeshindwa kutambua mahali walikofichwa mateka wake, wala kuwakamata makamanda mashuhuri wa Hamas kama Yahya Sanwar na Mohammad Dhaif.

Mauji ya halaiki ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina

Mbali na kushindwa kijasusi na kijeshi, imedhihirika wazi kuwa utawala huo wa kigaidi hauna uwezo wa kujilinda dhidi ya madola yenye nguvu kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ya uungaji mkono na msaada wa Marekani. Tarehe 1 Aprili, utawala wa Kizayuni ulishambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Syria, ambapo ulikabiliwa na jibu kali la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tarehe 14 Aprili.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilirusha mamia ya ndege zisizo na rubani na makombora kutokea ardhi yake kuelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (israel), ambapo utawala huo wa Kizayuni kwa msaada wa Marekani, Uingereza na Ufaransa ulijaribu kuzuia ndege na makombora hayo lakini idadi kubwa ya makombora ikafanikiwa kupenya na kupita kwenye mifumo yake ya ulinzi na kulenga shabaha zilizokusudiwa.

Kuhusiana na hilo, Azriel Bermant, mtafiti mkuu katika Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa mjini Prague, aliandika katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya jarida la Marekani la "Foreign Policy", kwamba uwezo wa nyuklia wa Israel haukuweza kuizuia Iran kuuadhibu kijeshi utawala huo." Mwaka 1991, Israel iliwaonya Wairaki kwamba kama wangeishambulia ingejibu kwa mashambulio makali ya nyuklia lakini hilo halikuwazuia Wairaki kurusha makombora ya Scud.

Shambulio la Iran la kuwaadhibu watu wenye misimamo mikali ya kupindukia mipaka huko Tel Aviv na katika Wizara ya Vita ya Israel, limeweka wazi ukweli wa kihistoria nao ni kwamba Israel haina uwezo wa kujilinda bila ya uingiliaji kati wa Marekani na washirika wake wengine, wakiwemo majirani na washirika wa Kiarabu. Bermant anasisitiza kwamba mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas na ya Aprili 14 ya Iran yamethibitisha wazi kwamba Israel haiwezi kujitegemea katika kukabiliana na maadui zake.

Tags