Onyo la viongozi wa China na Russia kwa Marekani kuhusu Afghanistan
Marais Vladimir Putin wa Russia na Xi Jinping wa China wametangaza baada ya mkutano wao huko Beijing kwamba Marekani na NATO zinabeba dhima ya matokeo ya uvamizi wao wa miaka 20 nchini Afghanistan na hazipaswi kujenga miundombinu ya kijeshi katika nchi hiyo.
Katika taarifa hiyo ya pamoja, pande hizo mbili zimesisitiza juu ya "kuimarisha ushirikiano na washirika kuhusiana na Afghanistan katika ngazi za pande mbili na kimataifa." Kwa mujibu wa marais hao lengo lao ni kuisaidi nchi hiyo iwe uhuru, inayojitegemea, yenye umoja, amani, isiyohusishwa na ugaidi wala dawa za kulevya na ambayo itakuwa na uhusiano mzuri na maelewano na majirani zake wote.
Misimamo ya viongozi wa China na Russia kuhusiana na Afghanistan inaonyesha wasiwasi wao mkubwa kuhusu sera za kijeshi za Marekani katika nchi hiyo. Kuruka ndege za kijasusi za Marekani na zisizo na rubani nchini Afghanistan, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa mara kwa mara na serikali ya Taliban nchini Afghanistan, kunaonyesha kuwa Marekani bado ina tamaa na Afghanistan na inajaribu kwa njia mbalimbali ikiwemo kushadidi ugaidi nchini humo, ili kuanda uwanja wa kurudi tena kijeshi nchini humo.
Hata hivyo, wasiwasi wa China na Russia kuhusu uwezekano wa kurudi jeshi la Marekani nchini Afghanistan unatokana zaidi na kusambaa ugaidi, biashara haramu ya magendo ya binadamu na ulanguzi wa dawa za kulevya na silaha kutoka Afghanistan kuelekea nchi za Asia ya Kati hadi kwenye mipaka ya China, kwa usimamizi wa jeshi la Marekani nchini Afghanistan. Ni kwa msingi huo ndipo awali Rais Vladimir Putin wa Russia akaonya kuhusiana na mjama za Marekani za kuibua migogoro, ikiwa ni pamoja na kuchochea hitilafu za kijamii kupitia uuzaji wa mihadarati nchini humo.
Akram Arefi, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema: "Kutokana na nafasi yake ya kistratijia katika eneo, Afghanistan daima imekuwa ikizingatiwa na kupewa muhimu na madola makubwa." Ingawa Marekani ilishindwa vibaya sana nchini Afghanistan na kulazimika kuondaka kwa madhili kutoka nchi hiyo kutokana na utamaduni wa kuchukiwa wageni wa kivamizi nchini humo, lakini kutokana na masuala ya kimkakati, bado inatamaa na nchi hiyo. Viongozi wa Russia na China huku wakitilia mkazo katika mkutano wao huko Beijing juu ya kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa Afghanistan na kuunga mkono ukarabati wa nchi hiyo, wamesisitiza kuwa Afghanistan inakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi na kijamii na kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kusaidia kutatua matatizo hayo. Jambo muhimu ambalo pande zote mbili zinalisisitiza ni kuachiliwa fedha za Afghanistan zinazoshikiliwa na Marekani. Serikali ya Washington imezuia takriban dola bilioni kumi ambazo ni mali ya wananchi wa Afghanistan na tayari imeshanyakua sehemu ya pesa hizo. Ni wazi kwamba kuachiliwa mali za watu wa Afghanistan kunaweza kutatua shida zao nyingi. Kuachiliwa kwa fedha hizo kunaweza kuwasaidia pakubwa watu hao ambao hivi sasa wanakabiliwa na matatizo chungu nzima yaliyosababishwa na mafuriko ya karibuni na wanahitajia misaada ya kimataifa.
Kauli ya Putin na Xi kuhusu siasa za kijeshi za Marekani nchini Afghanistan zinakuja huku nchi wanachama wa Jumuiya ya Makubaliano ya Usalama wa Pamoja na Russia, zimekuwa zikiituhumu Marekani kwa kujaribu kujenga miundombinu ya kijeshi nchini Afghanistan. Moja ya malengo muhimu ya Marekani nchini Afghanistan ni kuzusha vurugu na kuruga amani katika mipaka ya nchi hiyo na nchi za Asia ya Kati ikiwemo Tajikistan. Ni Kwa sababu hiyo ndipo, Russia pamoja na kuimarisha ulinzi wake katika mpaka na Tajikistan, ikazidisha ushirikiano wa kijeshi na kiusalama kati ya nchi za eneo la Eurasia.