UNRWA: Idadi ya Wapalestina waliolazimika kuihama Rafah imefikia 800,000
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i111938
Kwa mara nyingine tena karibu nusu ya Wapalestina wote waliokuwa Rafah, yaani watu wapatao laki nane hivi sasa wapo njiani wakilikimbia eneo hilo ambalo lilianza kushambuliwa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mei 6 baada ya kutolewa amri na jeshi hilo kuwataka watu wote waondoke katika eneo hilo.
(last modified 2024-05-19T10:44:31+00:00 )
May 19, 2024 10:44 UTC
  • UNRWA: Idadi ya Wapalestina waliolazimika kuihama Rafah imefikia 800,000

Kwa mara nyingine tena karibu nusu ya Wapalestina wote waliokuwa Rafah, yaani watu wapatao laki nane hivi sasa wapo njiani wakilikimbia eneo hilo ambalo lilianza kushambuliwa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mei 6 baada ya kutolewa amri na jeshi hilo kuwataka watu wote waondoke katika eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini imesema, wengi wa watu hao wanakimbilia eneo la katikati mwa Ghaza na Khan Younis ikiwemo katika majengo ambayo yameshambuliwa kwa makombora.

Katika taarifa aliyotoa kupitia mtandao wa kijamii wa X Lazzarini amesema: “tangu vita vianze huko Ghaza, Wapalestina wamelazimishwa kuyakimbia makazi yao mara kadhaa kwenda kusaka hifadhi katika maeneo salama ambayo hawajawahi kuyapata ikiwemo katika makazi ya UNRWA”.

Mkuu huyo wa UNRWA ameendelea kubainisha kuwa, watu wanapolazimika kukimbia wanaacha kila kitu chao na kuanza safari katika njia ambazo hazina usalama wala ulinzi.

Philippe Lazzarini

Ameongeza kuwa, Wapalestina hao huacha mahema, magodoro, vifaa vya kupikia na bidhaa nyingine muhimu kwa mahitaji ya binadamu ambazo hawawezi kubeba au kuzisafirisha; na kila mara wanapokimbia wanatakiwa kuanza upya.

Lazzarini amejibu pia taarifa za upotoshaji zinazotolewa kuhusiana na usalama wa wakimbizi Wapalestina kwa kusema: “madai kwamba watu wa Ghaza wanaweza kuhama kwenda maeneo ‘salama’ au ‘yenye mahitaji ya kibinadamu’ ni ya uongo. Kila mara, mazingira hayo yanaweka kwenye hatari kubwa maisha ya raia. Ghaza haina maeneo salama. Hakuna sehemu iliyo salama. Hakuna mtu aliye salama”.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa, kutokana na hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuzuia uingizaji misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza, hivi sasa hakuna chakula kilichosalia kwa ajili ya kuwagaia Wapalestina wa eneo hilo.../