Vyombo vya habari vinavyotumikia jinai (Google; mshirika katika jinai za Netanyahu)
-
Google mshirika katika jinai za Netanyahu
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi chetu cha Makala ya Wiki. Kipindi hiki kinachunguza dhulma ya vyombo vya habari kuanzia namna taarifa zilivyokusanywa na kufikishwa kwa watu hadi matangazo kuhusu kampeni za kipropaganda zilizofanywa na serikali ya Israel na kinafafanua ni kwa namna gani ueledi wa masuala ya vyombo vya habari na haja ya kuwepo uwazi vinaweza kudhihirisha uhakika na kuutoa chini ya vifusi vya upotoshaji. ******
Katika giza na kimya cha Gaza, ambapo maumivu na matumaini vimechanganyika pamoja, vyombo vya habari wakati mwingine hufanya kazi zake kama vioo vilivyovunjika; yaani hutoa taswira yenye mapungufu na iliyopotoshwa inayoficha uhakika wa mambo na hali halisi. Sauti za vilio vya watoto, machozi ya akina mama na ghadhabu za akina baba hupotea katika kelele za habari na kuwa simulizi zinazokataa kusema ukweli uliojeruhiwa. Dhulma ya vyombo vya habari ni jeraha baya sana la dunia ambalo halina tiba isipokuwa mtazamo wa wazi wa walimwengu.
Tangu kuasisiwa kwa utawala bandia wa Israel hadi sasa zaidi ya watu laki moja wasio na hatia wameuawa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi. Katika miongo ya karibuni, Wapalestina na raia wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza wamekabiliwa na vikwazo vikubwa na kuzingirwa kikamilifu mbali na ardhi yao kukaliwa kwa mabavu na kuuliwa kiholela. Hali ya sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ni matokeo ya zaidi ya miongo 7 ya sera za Israel za kuvamia na kuwaua raia wa Palestina wasio na hatia. Mashine hii ya mauaji ya Wazayuni imekuwa ikiendelea kufanya kazi yake kila siku, lakini tangu Hamas ilipotekeleza Oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa, tarehe 7 Oktoba 2023, na baadaye hujuma kubwa na mauaji ya kimbari ya Israel ambapo imetumia nguvu zote za jeshi dhidi ya raia na watoto wa Kipalestina, tumeshuhudia jinai kubwa za utawala huo dhidi watu wasio na hatia wa Palestina ambao kwa miaka mingi wamevumilia na kustahamili mateso yasiyo na kifani. Wananchi ambao wanaishi katika jela ya wazi, na mbali na kuathiriwa na njaa waliyosababishiwa kwa makusudi, kiu, kukosa huduma muhimu kama umeme, maji, dawa, misaada ya kibinadamu na n.k, wamestahamili pia mashambulizi ya ndege za kivita, kuuawa marafiki na familia zao na kubomolewa nyumba na miji yao. Jinai hizi zimemgusa na kumuathiri kila binadamu baada ya kuchapishwa baadhi tu ya picha kuhusu mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Haya yote yanatufanya tujiulize swali muhimu kwamba: Ni kwa kiasi gani vyombo vya habari vimekuwa na taathira katika kuwadhihirisha Wazayuni kuwa ni watu waliodhulumiwa, na vilevile katika kuhalalisha jitihada za utawala huo chinja chinja wa watoto za kuficha jinai zake n.k.?
Katika dunia ya leo, mashirika na vyombo vya habari na teknolojia kama Google, Facebook (Meta) na makampuni mengine makubwa ya kidijitali yana mchango mkubwa ambao ni zaidi ya kutoa huduma ndogo na nyepesi za kusachi maudhui au mawasiliano ya kijamii. Makampuni haya yamekuwa zana zenye nguvu za kuendeleza malengo ya kiuchumi, kitamaduni, kijamii, na kisiasa kutokana na ufikaji wao mpana kwa hadhira, wingi wa data za watumiaji, na uwezo wa kudhibiti mtiririko wa taarifa na habari. Katika uwanja wa uchumi na biashara, Google na mfumo wake wa utangazaji, inaruhusu biashara na wafanyabiashara kutambua wateja kulingana na sifa za kitabia, eneo la kijiografia, na maslahi binafsi. Katika uga wa kiuatamduni na kielimu, mifumo kama Google Scholar na YouTube imetoa jukwaa kwa ajii ya uchapishaji na kupata elimu kwa uhuru. Aghalabu ya vyuo vikuu na taasisi za elimu zinatumia zana hizi kuendesha kozi mbalimbali kwa njia ya mtandao, kuchapisha marejeo ya elimu na kuendeleza utamaduni wa kidijitali.
Lakini labda kipengele chenye utata zaidi cha kutumia makampuni kama Google ni kuendeleza malengo ya kisiasa. Uwezo wa Google katika kuelekeza fikra za waliowengi kupitia vigezo vya utafutaji na propaganda iliyoratibiwa kwa malengo maalumu umezingatiwa sana duniani. Namna Google inavyoonyesha matokeo ya utafutaji inaweza pia kutilia mkazo simulizi fulani za kisiasa.
Google pia ina nafasi muhimu katika upande wa sera za nje na diplomasia ya dijitali. Nchi mbalimbali hujaribu kuwasilisha taswira chanya ya utamaduni, siasa au uchumi wao kwa ulimwengu kwa kuboresha maudhui ya kidijitali (SEO) na kuchapisha maudhui yenye mwelekeo maalumu kwenye mifumo inayomilikiwa na Google. Mbinu hii ni aina ya "nguvu laini" ambayo inaweza kuwa na ufanisi katika kuboresha taswira ya kimataifa ya nchi mbalimbali. Mfano wenye utata wa jinsi siasa zinavyotumia vibaya data za kidijitali ni kadhia ya Cambridge Analytica katika uchaguzi wa Marekani. Ingawa tukio hilo lilihusiana zaidi na Facebook, lakini limeonyesha namna data za watumiaji zinavyoweza kuathiri matokeo ya uchaguzi. Google pia inachunguzwa mara kwa mara na weledi wa masuala ya kisiasa kutokana na shughuli zake zinazofanana na hizo.
Licha ya fursa hizo, kutumiwa mashirika makubwa ya habari kwa ajili ya malengo ya kisiasa na kiuchumi kumekabiliwa na changamoto kubwa. Kurundikana taarifa kwenye makampuni kadhaa ambako hakujawahi kushuhudiwa, kumeibua wasiwasi kuhusu faragha, uwazi na uwezekano wa kupotoshwa mtiriko wa taarifa na habari.
Hata hivyo simulizi za siku hizi ni kuhusu tuhuma zinazoikabili Google na vyombo vya habari katika kusimamia maudhui za habari, kudhibiti mtiriko wa habari na kuibua taarifa zilizopotoshwa dhidi ya Gaza; kwa kadiri kwamba kufutwa au kuchujwa video na picha halisi kuhusu ukandamizaji na mateso ya watu wa Gaza kumepelekea kuibuliwa uwongo na kupotoshwa taarifa za kweli. Wakosoaji wanaamini kwamba kitendo cha Google cha kuzuia taarifa halisi kwa walimwengu na kusaidia kueneza taarifa za upendeleo kimechangia kwa njia fulani kuenea habari za uwongo kuhusu wananchi madhulumu wa Ukanda wa Gaza. Hivyo vyombo vya habari vilivyo huru na vinavyofanya kazi kwa uwazi vina jukumu muhimu la kuakisi uhakika mchungu wa katika eneo hili.
Hivi karibuni tovuti ya Drop Site News ilifichua kuwa Google ilitia saini makubaliano ya dola milioni 45 na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ili kueneza taarifa za Tel Aviv na kupuuza jinai walizotendewa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza katika muda wa siku 700. Haya ni miongoni mwa maafa binadamu yaliyoendelea kwa muda mrefu sana katika dunia ya sasa.
Drop Site News imeripoti kuwa, kampuni ya Google inachangia kueneza jumbe za serikali ya Israel na kuarifisha mgogoro wa binadamu unaowakabili Wapalestina wa Ukanda wa Gaza kwa mujibu wa makubaliano ya miezi sita iliyofikia na Netanyahu yenye thamani ya dola milioni 45.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, makubaliano hayo yalitiwa saini mwishoni mwa mwezi Juni mwaka jana na imeitaja kampuni ya Google kama "upande mkuu" unaounga mkono mkakati wa mahusiano ya umma wa Netanyahu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matangazo yanadhibitiwa kupitia YouTube na katika jukwaa la "Google Display & Video 360" hutajwa katika hati za serikali ya Israel kama "Hasbara", neno la Kiebrania ambalo aghalabu hufasiriwa kama kampeni.
Wakati huo huo rekodi zinaonyesha kuwa Israel pia ilitumia dola milioni tatu kwa ajili ya kurusha matangazo yake katika jukwa la kampuni ya Kimarekani ya "X" na dola milioni 2.1 kupitia jukwaa la Israel la "OutBrain."
Msemaji wa jeshi la utawala ghasibu wa Israel wakati huo alieleza kuwa: "Maafisa wa serikali wanaweza kuanzisha kampeni ya kidijitali ili kueleza kwamba hakuna sera za kusababisha njaa huko Gaza na kuwalisha data zao."
Tangu wakati huo, serikali ya Israel imeendesha pakubwa kampeni zake ambazo zinapinga suala la kuwepo njaa miongoni mwa wakazi wa ukanda huo ikiwemo video iliyotumwa YouTube na Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Israel ambayo maudhui yake yanadai kuwa kuna chakula huko Gaza, na madai yoyote mengine ni ya uwongo.
Video hiyo ilitazamwa na watu zaidi ya milioni 6 na sehemu yake kubwa imepakuliwa kupitia matangazo yenye mwelekeko maalumu.
Tel Aviv imezidisha mbinu za kipropaganda ili kueneza taarifa za uwongo huku Israel ikiendelea kulaaniwa pakubwa kimataifa kwa hatua yake ya kuvifunga vivuko vyote vinavyoelekea Gaza mnamo tarehe pili Machi iliyopita. Hii ni katika hali ambayo Israel ilizuia kuingizwa bidhaa zote za chakula, dawa za matibabu au misaada ya kibiandamu na imelisababishia kwa makusudi njaa eneo hili licha ya mlundikano wa malori ya misaada katika mipaka yake.
Propaganda hizo za upotoshaji zinaendeshwa na utawala wa Kizayuni kwa kushirikiana na makampuni makubwa huku dunia ikishuhudia na kuthibitisha namna utawala huo unavyotumia njaa kwa makusudi kama silaha ya vita. Aidha kwa mujibu wa ripoti kadhaa za filamu za matukio ya kweli kuhusu jinai za mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza, hivi karibuni jumuiya ya kimataifa ya wasomi na wataalamu wa mauaji ya kimbari ilitaja hatua za serikali na jeshi la Israel huko Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu.
Na mwisho kabisa tunaweza kusema kuwa makampuni ya vyombo vya habari na teknolojia kama Google yamekuwa wenzo muhimu wa kufanikisha malengo maalumu katika nyanja mbalimbali. Kutumiwa suhula na uwezo wa makampuni hayo kwa umakini na kwa kuwajibika kunaweza kuchangia ustawi wa kiuchumi, kiutamduni na hata ushiriki wa kidemokrasia lakini kupuuzwa na kukosekana usimamizi wa kutosha kunaweza kuwa sababu ya kutumiwa vibaya suhula hizo na hivyo kutishia uhuru wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.