Russia: Magharibi inacheza na moto
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametangaza kwamba nchi za Magharibi zinataka kuzidisha mvutano na zinacheza na moto kwa kuipatia silaha na kuihimiza Ukraine kushambulia ardhi ya Russia.
Onyo la Moscow limetolewa sambamba na kushadidi mashambulizi ya Ukraine dhidi ya miji ya Russia, huku Kiev ikipoteza baadhi ya maeneo ya Kharkiv katika vita vyake na Russia.
Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kutumwa kwa silaha za nchi za Magharibi nchini Ukraine, amesema: "Wameipatia Kiev makombora ya masafa marefu na silaha nzito, na kuiwashia taa ya kijani ya kutumia silaha hizo dhidi ya Russia." Amongeza kuwa, "sifa za maafisa wa Marekani na Uingereza wanaosimamia mashambulizi haya ya kikatili zinaonekana wazi."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa: "Moscow inazionya Washington, London, Brussels (Umoja wa Ulaya) na Kiev, ambayo iko chini ya udhibiti wao, kwamba wanacheza na moto, kwa sababu Russia itajibu uchokozi kama huo katika ardhi yake."
Siku za Alhamisi na Ijumaa wiki hii, jeshi la Ukraine lilishambulia huko Crimea, Krasnodar na mikoa mingine ya Russia kwa kutumia ndege zisizo na rubani. Wizara ya Ulinzi ya Russia inasema, ilifanikiwa kutungua zaidi ya drone mia moja ya Kiukraine.