May 10, 2024 02:08 UTC
  • Madai ya Marekani ya kusimamisha kuupelekea silaha utawala wa Kizayuni wa Israel

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alidai siku ya Jumatano mbele ya Baraza la Seneti la nchi hiyo kwamba kuupelekea silaha utawala wa Kizayuni wa Israel kumesimamishwa kwa sababu ya utawala huo kutekeleza operesheni ya kuivamia kijeshi Rafah, lakini pamoja na hayo bado hawajachukua uamuzi rasmi kuhusu hatima ya shehena hiyo ya silaha.

Mkuu huyo wa Pentagon amedai kwamba Marekani ilishaieleza bayana Israel kuwa inapaswa kuwazingatia raia katika utekelezaji wa operesheni yake ya kijeshi, na akasisitiza kwamba Washington haitaki kuona operesheni kubwa ya kijeshi inafanywa katika mji huo na kwamba juhudi zote zielekezwe katika kuwalinda raia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller alisema Jumatano usiku kwamba Washington haijaidhinisha shambulio la Israel dhidi ya Rafah na akazungumzia kusitishwa mpango wa kuipelekea Israel mabomu ya pauni 2,500 kwa kusema: "tumesimamisha usafirishaji wa shehena ya msaada wa muda mfupi na tunaendelea kuchunguza shehena nyinginezo."

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Joe Biden alidai katika msimamo mpya aliotangaza Jumatano hiyohiyo usiku kwenye mahojiano na CNN kwamba ikiwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ataamuru kufanywa mashambulizi makubwa dhidi ya Rafah katika Ukanda wa Ghaza, atasimamisha upelekaji wa silaha za Marekani kwa utawala huo. 

Biden aliongezea kwa kusema: "nilitangaza wazi kwamba ikiwa (Israel) wataingia Rafah - hadi sasa hawajaingia Rafah - sitadhamini silaha ambazo kihistoria, zinatumika kuhusiana na Rafah na miji mingine."

Biden aliendelea kueleza kuwa Marekani itaendelea kuidhaminia Israel silaha za kiulinzi ikiwa ni pamoja na mtambo wa ulinzi wa anga wa Kuba la Chuma, lakini itazuia kuipatia silaha zingine iwapo itaanzisha mashambulizi makubwa ya ardhini dhidi ya Rafah.

Gilad Erdan, balozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa ametoa mjibizo kwa uamuzi uliotangazwa na Marekani wa kusimamisha kwa muda upelekaji wa shehena ya silaha kwa Israel kufuatia mashambulizi ya ardhini yaliyofanywa na utawala huo dhidi ya Rafah, akisema "unavunja moyo sana".

Madai ya Marekani kuhusu kusitishwa upelekaji silaha kwa Israel, ambao kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo hadi sasa umefanywa kuhusiana na shehena moja ya silaha, yanaonyesha kuwa Ikulu ya White House imeamua kutumia wenzo wa shinikizo dhidi ya Netanyahu ili kumlazimisha abadilishe mkakati wake kuhusu vita vya Ghaza.

Kwa muda sasa, Washington na Tel Aviv zimekuwa zikihitilafiana kuhusu namna ya kuendelezwa operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni huko Ghaza hususan mvutano ambao umekuwepo kati ya Washington na baraza la vita la Israel kuhusu uwezekano wa jeshi la utawala huo kufanya shambulio dhidi ya mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ghaza.

Netanyahu, ambaye amefungamanisha hatima yake ya kisiasa na vita vya Ghaza, akiwa ametoa ahadi nyingi tangu ulipoanza uvamizi wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza, ikiwemo ya kuwakomboa mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa makundi ya Muqawama na kuyaangamiza makundi ya Muqawama hususan la Hamas, hivi sasa, na baada ya kupita miezi saba tangu vilipoanza vita hivyo amekikwaa kisiki kikubwa; na anavyohisi mwenyewe njia pekee ya kujinasua na hali hiyo ni kuishambulia kijeshi Rafah kwa madai ya kuangamiza mabaki ya wanachama wa Hamas na makundi mengine ya Muqawama na kuwakomboa mateka wa Kizayuni.

Kuhusiana na suala hili, tangu siku kadhaa zilizopita, jeshi la Kizayuni limefanya mashambulizi makubwa ya anga na ardhini huko Rafah na kuwataka wakazi wa Ghaza, -ambao walikimbilia mji huo kutafuta hifadhi baada ya kuteketezwa maeneo ya kaskazini na ya katikati ya Ukanda wa Ghaza-, sasa wahame Rafah na kuhamia maeneo mengine.

Hata hivyo, kwa kuzingatia mrundikano mkubwa wa watu uliopo huko Rafah, shambulio lolote kubwa la ardhini litakalofanywa kwenye mji huo litasababisha maafa makubwa ya roho za watu; na ndio maana Umoja wa Mataifa umetoa indhari kali juu ya kufanywa shambulio kama hilo na matokeo mabaya yatakayotokezea. Maoni sawa na hayo yametolewa hata kwenye vyombo vya utawala vya Marekani. Seneta Dick Durbin, Mkuu wa Kamati ya Sheria ya Seneti ya Marekani amesema, ni "vigumu" kutetea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na ametaka utawala huo uheshimu viwango vya masuala ya kibinadamu.

Kutokana na upinzani mkubwa wa kimataifa dhidi ya mashambulizi makubwa ya ardhini ya jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya Rafah na kutokuwepo na hoja ya kuhalalisha hatua hiyo, hivi sasa Washington imelazimika kuchukua msimamo usio wa kawaida wa kutishia kusimamisha upelekaji silaha kwa Israel bali hata kusimamisha shehena moja ya silaha hizo. Kabla ya hapo, katika barua waliyomwandikia Rais wa nchi hiyo Joe Biden, wawakilishi 88 wa chama cha Democratic katika Bunge la Marekani walikuwa wameomba uuzaji wa silaha za kushambulia kwa Israel upigwe marufuku.

Wakati huo huo, kuendelea maandamano ya wanafunzi nchini Marekani, ambayo yameenea sana na kwa namna ambayo haijawahi kutokea, kumeulazimisha utawala wa Biden ubadili msimamo wake wa kila siku, ambao ni kutoa uungaji mkono wa pande zote za kisiasa na kijeshi kwa Tel Aviv.  

Vuguvugu kubwa la wanafunzi nchini Marekani la kuwaunga mkono Wapalestina limeanza na linaendelea katika hali ambayo misimamo kadhaa imeonyeshwa ndani ya Bunge la Kongresi ya kupinga jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na uungaji mkono wa serikali ya Marekani kwa jinai hizo.

Seneta wa kujitegemea Bernie Sanders alituma ujumbe wa X kumhutubu waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu- aliyewatuhumu wanafunzi wa Marekani kwamba wanaeneza chuki dhidi ya Wayahudi-, akimwambia: "hapana, Bwana Netanyahu, hizi sio chuki dhidi ya Wayahudi. Katika muda wa zaidi ya miezi sita, baraza lako la mawaziri lenye misimamo ya kufurutu mpaka limewaua Wapalestina 34,000 na kuwajeruhi zaidi ya 77,000, na 70% ya waathirika hawa ni wanawake na watoto wa Ghaza".

Bernie Sanders

Lakini mbali na hayo, wakati huu wa kuelekea uchaguzi wa rais utakaofanyika mwezi Novemba, timu ya kampeni ya Joe Biden ina wasiwasi mkubwa juu ya kupungua mno kura za kiongozi huyo miongoni mwa wapiga kura wa jadi wa chama cha Democratic, yaani vijana, Wamarekani wa jamii za wachache na wanawake kutokana na msimamo na hatua zake za kuuunga mkono utawala wa Kizayuni katika vita vya Ghaza.

Suala jingine muhimu ni kukiri Biden mwenyewe kuhusu namba silaha za Marekani zilivyochangia katika vita vya Ghaza na mauaji ya Wapalestina. Katika mahojiano yake na CNN, Biden ameashiria mabomu ya pauni 2,000 ambayo Marekani imeipatia Israel na kusema: "raia wa Ghaza wameuawa kwa mabomu haya".

Katika miezi ya karibuni, Marekani, ambayo ni muungaji mkono wa pande zote wa Israel, imeipatia Tel Aviv shehena za silaha na kila aina ya risasi ili kuwashambulia watu wanaodhulumiwa wa Ghaza, na hivi karibuni iliidhinishwa pia katika bunge la nchi hiyo na kusainiwa na Joe Biden ili kuwa sheria, bajeti ya msaada wa kijeshi wa dola bilioni 26 kwa utawala huo wa Kizayuni.

Kutokana na yote hayo, kuna kila sababu ya kuitambua Marekani kama mshirika katika jinai za utawala wa Kizayuni katika vita vya Ghaza na mauaji ya kimbari ya Wapalestina.../

 

Tags