May 09, 2024 12:23 UTC
  • Rais wa Marekani: Nimeupata ujumbe wa wanafunzi wanaounga mkono watu wa Palestina

Baada ya zaidi ya wiki tatu za maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani na wahadhiri wanounga mkono taifa la Palestina, Rais Joe Biden wa nchi hiyo amesema ameupata ujumbe wao.

Maandamano ya wanafunzi wanaounga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel yaliyoanzia hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York, Marekani, yameenea katika vyuo vikuu vingine vya nchi hiyo na maeneo mengine ya dunia, licha ya kuendelea ukandamizaji wa viongozi na idara za nchi hiyo dhidi ya wanachuo.

Rais Joe Biden wa Marekani anadai kupata na kusikia ujumbe wa wanafunzi, wahadhiri na wasomi wanaoandamana kupinga jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina, baada ya kuuawa shahidi karibu watu 35,000 huko Gaza na zaidi ya wiki tatu za maandamano ya wanafunzi, wahadhiri na wasomi wanaoandamana kuunga mkono taifa la Palestina.

Wanafunzi wakiandamana kutetea Wapalestina

Akidai kuwa Israel bado haijavuka mstari mwekundu kuhusiana na Rafah, Biden amesema akiunga mkono utawala wa Kizayuni kwamba Marekani itaendelea kuihakikishia Israel usalama na uwezo wake wa kujilinda kwa kutumia ngao ya kutungua makombora ya Iron Dome na kujibu mashambulizi ya adui.

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023 utawala wa kimbari wa Israel ukiungwa mkono kikamilifu na Marekani na nchi za Magharibi unaendeleza mauaji makubwa ya umati katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya raia wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina.

Hadi sasa zaidi ya Wapalestina elfu 34 800 wameuawa shahidi na zaidi ya wengine elfu 78 na 400 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama.

Tags