May 10, 2024 02:10 UTC
  • Iran: Tutaangalia upya sera ya nyuklia iwapo uwepo wetu utatishiwa

Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu italazimika kuangalia upya kanuni yake ya nyuklia iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utatishia uwepo na usalama wa taifa hili.

Kamal Kharrazi ameyasema hayo katika mahojiano na Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar na kuongeza kuwa, iwapo Israel itafanya makosa na iharibu vituo vya nyuklia vya Iran, basi Jamhuri ya Kiislamu haitakuwa na budi kutoa jibu 'tofauti'.

Amesema, "Miaka miwili iliyopita katika mahojiano na al-Jazeera, nilisema kuwa Iran ina uwezo wa kuzalisha bomu la nyuklia, na leo hii tungali tuna uwezo huo; lakini hatujafikia uamuzi wa kuunda bomu la nyuklia."

Ikumbukwe kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umesema mara chungu nzima kwenye ripoti zake kwamba Iran haina ratiba zozote za kumiliki silaha za atomiki na kwamba mradi wake wa nyuklia ni wa amani kikamilifu. 

Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haina nia ya kuunda silaha za nyuklia na inachofuatilia siku zote ni nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.

Kuhusu uhusiano wa Iran na Saudi Arabia, Kharrazi amebainisha kuwa, kuhuishwa uhusiano wa Tehran na Riyadh ilikuwa hatua nzuri yenye maslahi kwa mataifa haya mawili.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haiitambui Israel, na inauona utawala huo kuwa utawala ghasibu unaoua, kupora ardhi, nyumba na mali za Wapalestina.

Tags