May 08, 2024 08:13 UTC
  • Kujiweka tayari Wayemen kwa ajili ya kuuzingira utawala wa Kizayuni baharini

Tovuti ya habari ya Ansarullah ya Yemen imeripoti kuwa, jeshi la nchi hiyo limeanza kuratibu operesheni ya pili ya awamu ya nne ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni sambamba na kuanza mashambulizi ya utawala ghasibu wa Kizayuni katika mji wa Rafah.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, meli za kampuni yoyote ya kimataifa ambazo zitakuwa zinaelekea  katika bandari za utawala wa Kizayuni zitajumuishwa katika orodha ya shabaha za jeshi la Yemen, na usafirishaji wao utapigwa marufuku ndani ya eneo la shughuli za jeshi la Yemen.

Utekelezaji wa hatua ya nne unamaanisha kushambuliwa meli zote zinazokwenda katika bandari za Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) bila ya kujali utaifa wa meli hizo na katika bahari zote, ikiwemo Bahari ya Mediterania. Hii ni pamoja na kuwa awamu ya nne ya harakati za jeshi la Yemen inafanyika katika fremu ya  kuimarisha uwezo na nguvu za mhimili wa muqawama katika nyanja zote.

Operesheni ya Jeshi la Yemen 

Kwa hakika, kushiriki Yemen katika vita kwa maslahi ya wakazi wa Gaza ndio maana halisi ya umoja katika medani za vita yaani kukabiliana na adui katika nyanja zote. Kufuatia tangazo la kuingia Yemen katika awamu ya nne ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Ghaza, Zaifullah Al-Shami, Waziri wa Habari wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa Yemen ina uwezo ambao unaipa ujasiri wa kusimama katika mstari wa mbele wa kuunga mkono taifa la Palestina, na hivi karibuni idadi ya wapiganaji walio tayari kujiunga katika vita hivyo itaongezeka na kufikia watu milioni moja.

Katika kuunga mkono Gaza, Yemen imekwamisha juhudi za Marekani na Uingereza za kuvunja mzingiro uliouwekea utawala wa Kizayuni katika eneo la Bahari Nyekundu kwa kuanzisha mashambulizi yake tarehe 31 Oktoba ambapo imetekeleza makumi ya operesheni dhidi ya adui. Baada ya shambulio la nchi kavu la jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza, jeshi la Yemen lilitangaza kuwa litalenga meli za Israel na nyinginezo zinazoelekea katika bandari za Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni katika kuunga mkono makundi ya wanamuqawama na wananchi wa Palestina ambapo katika kipindi hicho, mbali na kulenga meli hizo pia imefanikiwa kunasa kadhaa miongoni mwazo.

Jeshi la Yemen likijaribu kusimamisha meli inayoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Kutokana na operesheni hizo, bandari ya Eilat katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu imefungwa na utawala wa Israel kulazimika kutumia njia mbadala.

Jarida la Ujerumani la Spiegel limefichua ripoti ya mkutano wa siri uliofanyika mjini Brussels, ambapo kamanda wa wanamaji wa Umoja wa Ulaya alikiri kuhusiana na uwezo mkubwa wa jeshi la Yemen katika Bahari Nyekundu. Admeri Vasilius alisema katika mkutano huo kwamba: 'Sisi tunatumia mifumo ya kisasa kabisa ya ulinzi, lakini pamoja na hayo mifumo hiyo yenye nguvu kubwa inasalimu amri mbele ya kundi kubwa la ndege zisizo na rubani za Yemen.'

Kwa msingi huo, tunaweza kusemwa kuwa, hatua ya Netanyahu kupuuza maonyo ya Yemen ya kuepuka kuishambulia Rafah kutausababishia utawala huo na waungaji mkono wake yaani Marekani na Uingereza, gharama kubwa zisizotarajiwa, isipokuwa iwapo nchi hizo zitaacha kuunga mkono utawala huo na kumshinikiza Netanyahu na baraza lake la vita wasimamishe vita mara moja.