May 18, 2024 03:58 UTC
  • Putin: Kwa sasa hakuna mpango wa kuuteka mji wa Kharkiv huko Ukraine

Rais wa Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa operesheni za mapigano katika eneo la Kharkiv nchini Ukraine zinalenga kuanzisha "ukanda salama" utakaozuia mashambulizi Ukraine kufika katika ardhi ya Russia.

Akizungumza jana Ijumaa katika mkutano na vyombo vya habari katika mji wa Kharbin nchini China, Rais Putin alisema kuwa Moscow kwa sasa haina mpango wa kuuteka mji wa Kharkiv huko Ukraine. 

Rais wa Russia amesema kuwa, Ukraine imekuwa ikifanya mashambulizi katika makazi ya raia katika maeneo ya mipakani ikiwa ni pamoja na mji wa Belgorod na kwamba raia wanapoteza maisha katika hujuma hizo za Ukraine. 

Rais Vladimir Putin amesema kuwa alitamka hadharani kwamba iwapo mashambulizi ya Ukraine yataendelea katika maeneo hayo Russia itaanzisha eneo salama; na kwamba hicho ndicho wanachokifanya sasa. 

Akiwa ziarani nchini China, Rais Putin amesema kuwa  amejadiliana na mwenzake wa nchi hiyo, Xi Jinping kuhusu njia za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Ukraine na kuongeza kuwa, Beijing imedhamiria kusuluhisha mzozo kati ya Moscow na Kyiv.  

Rais Putin akizungumza na Jinping mjini Beijing 

Wakati huo huo, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine ameitaja hali ya mapigano katika mji wa Kharkiv nchini humo kuwa ngumu sana, na amekutana na wakuu wa jeshi la nchi hiyo kujadili hatua wanazoweza kuchukua mkabala wa hali hiyo.

Tags