May 31, 2024 07:28 UTC
  • Barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wanachuo wa Marekani wanaotetea Palestina

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika barua aliyowaandikia wanachuo wenye utu wanaotetea wananchi wa Palestina katika vyuo vikuu vya Marekani, ameonyesha mshikamano wake na maandamano ya wanachuo hao dhidi ya uzayuni na kuwataja kuwa sehemu ya mrengo wa muqawama.

Ameashiria hali inayozidi kubadilika ya hatima ya eneo la Asia Magharibi na kusisitiza mabadiliko ya kihistoia yanayoendelea kutokea ulimwenguni. Barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wanachuo wa Marekani wanaotetea Palestina ina umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani mienendo isiyo na mifano yake ya uungaji mkono kwa kadhia ya Palestina na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina, katika nchi za Magharibi hususan Marekani. Mashambulio ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina na kuendelea jinai za kutisha na zisizo na mfano wake zinazofanywa na utawala huo katika ukanda huo, ambazo sasa zinakaribia kutimiza mwezi wa nane, kumeibua wimbi kubwa zaidi la maandamano ya wanachuo kuwahi kushihudiwa tangu kuanza maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani mwaka 2020. Mbali na wanachuo, kwa mara ya kwanza, idadi kubwa ya wahadhiri na wakuu wa vyuo vikuu wamejiunga na maandamano ya wanachuoi huko Marekani kwa ajili ya kuunga mkono na kutetea Palestina. Maandamano hayo yanayaweza kuchukuliwa kuwa ni jambo jipya katika mfumo wa kisiasa na kijamii katika nchi hiyo. Ni wazi kuwa maandamano hayo pia yameenea katika nchi za Ulaya.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika barua yake Ayatullah Khamenei amewaambia vijana wa Marekani ambao dhamiri zao zimeamka na kuwasukuma wawatetee watoto na wanawake wanaodhulumiwa wa Gaza kuwa mbali na maandamano yao katika makumi ya vyuo vikuu vya Marekani, vyuo vikuu na watu wa nchi nyingine pia wamesimama kuwatetea watu wa Palestina wanaoendelea kuuawa kwa umati na Wazayuni. Amewaambia: "Hatua ya wahadhiri ya kukuungeni mkono nyinyi wanachuo ni tukio muhimu na lenye taathira kubwa, ambalo linaweza kuchangia pakubwa katika kupunguza machungu ya ukandamizaji wa polisi na mashinikizo yanayotolewa dhidi yenu. Mimi pia ninashikamana na nyinyi vijana na kupongeza mapambano yenu."

Maandamano makubwa na yasiyo na mfano wake ambayo yanashuhudiwa katika vyuo vikuu vya Marekani kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina na kupinga vitendo vya jinai vya Israel kwa mara nyingine tena yanaashiria mabadiliko ya kimsingi na muhimu katika mtazamo wa kizazi cha vijana wa Marekani kuhusu suala zima la Palestina. Sasa swali hili linaulizwa tena na tena kuwa je, ni kwa nini kizazi cha vijana, au kwa ibara sahihi zaidi, "Generation Z", tofauti na walivyo baba zao, wanaiunga mkono Palestina na hawauhurumii tena utawala wa kibaguzi wa Israel? Viongozi na taasisi zilizo karibu na lobi za Wazayuni huko Marekani, pamoja na watawala wa Tel Aviv, wamejaribu kupotosha ukweli wa chanzo cha malalamiko na maandamano ya wanachuo wa Marekani na kudai kuwa yanatokana na  kupotoshwa kizazi kipya cha vijana wa Marekani na hivyo kutaka vikosi vya usalama viwakandamize bila huruma. Ubeberu wa vyombo vya habari vya Magharibi ambao unautumikia kikamilifu utawala wa Kizayuni, unafanya kila unaloweza kwa ajili ya kufunika jinai za utawala huo na kuonyesha kuwa unadhulumiwa.

Wanachuo wanaoiunga mkono Palestina, wakiwemo wa Kiyahudi wanaopinga vitendo vya jinai na mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza, wanasema wanatuhumiwa visivyo kuwa wanaeneza chuki dhidi ya Mayahudi kwa sababu tu ya kuikosoa Israel na kuunga mkono haki za binadamu. Mfumo unaotawala Marekani unawakandamiza vikali wale wanaotuhumiwa kueneza chuki dhidi ya Mayahudi na kuwatetea Wapalestina, hivyo tunaweza kusema kuwa waandamanaji wanatoa muhanga maisha yao ya baadaye kwa ajili ya kueteta malengo yao matukufu ya kiutu.

Katika barua yake hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezingatia kwa kina namna utawala haramu wa Kizayuni ulivyoundwa na jinai zake dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina pamoja na nafasi ya Marekani na nchi nyingine za Magharibi katika kutetea vitendo vya kikatili vya Israel, na kuwahutubu wanachuo wanaotetea Palestina huko Marekani kuwa sasa wamesimama upande sahihi wa historia - ambayo inaendelea kubadilika. Huku akiendelea kufichua utambulisho halisi wa Israel, amesema utawala wa Kizayuni tangu uasisiwe unekuwa ukitumia siasa za "mkono wa chuma" dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina na kupuuza dhamiri, thamani za kibinadamu na kidini na kuongeza ukatili na ugaidi wake siku baada ya siku. Marekani na washirika wake hawajaonyesha kuchukizwa hata kidogo na ugaidi huo wa serikali ya Kizayuni dhidi ya watu wasio na hatia. Hata leo, baadhi ya kauli za serikali ya Marekani kuhusiana na jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa kibaguzi wa Israel huko Gaza ni za kinafiki tu na zisizo na ukweli wowote.

Ayatullah Khamenei amebainisha nafasi ya Marekani katika kudumisha uhai wa utawala wa Kizayuni na kuandika katika barua yake kwamba, muungaji mkono mkubwa wa utawala huo ghasibu baada ya misaada ya kwanza ya Waingereza ni Marekani ambayo inaendelea kutoa misaada ya kila aina ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi kwa utawala huo na hata kuuwezesha kutengeneza silaha za maangamizi ya umati za nyuklia.

Suala jingine muhimu katika barua ya Ayatullah Khamenei kwa wanachuo wa Marekani ni kuashiriwa nafasi ya mhimili wa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni. Ameandika kwamba: "Mrengo wa Muqawama" uliibuka kutoka kwenye kitovu cha mazingira haya yenye giza na hali ya kukata tamaa na kupelekea kuundwa serikali ya "Jamhuri ya Kiislamu" nchini Iran, mrengo ambao unaendelea kuenea na kupata nguvu zaidi."

Mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina

Sasa Mrengo huo wa Muqawama umepata wigo wa kimataifa. Kuhusiana na hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika barua yake akiwahutubu wanachuo wa Marekani wanaounga mkono Palestina kwamba: "Hivi sasa ninyi mnaunda sehemu ya muqawama, na chini ya mashinikizo ya kikatili ya serikali yenu - ambayo inautetea waziwazi utawala ghasibu na katili wa Kizayuni - ambapo mmeanzisha mapambano ya heshima na utukufu dhidi ya utawala huo. Mrengo mkubwa wa Muqawama umekuwa ikipigana kwa miaka mingi katika eneo la mbali, ukiwa na utambuzi na hisia hizi hizi mlizonazo leo."

Nukta nyingine iliyo wazi katika barua hii ni ishara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu vita vya kisaikolojia vinavyoendeshwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na Uzayuni na juhudi zao za kuwasilisha picha potofu ya matukio ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuwafanya madhalimu waonekane kuwa ndio wanaodhulumiwa. Katika barua hii, Kiongozi Muadhamu ameandika kwamba viongozi wa Uzayuni wa kimataifa, ambao wanamiliki mashirikai mengi ya vyombo vya habari huko Marekani na Ulaya au wameyahonga mashirika hayo, wanapotosha ukweli kwa makusudi kwa kuyatuhumu mapambano na muqawama huo wa kishujaa unaopigania thamani za kibinadamu kuwa ni ugaidi! Je, taifa linalopigana katika ardhi yake dhidi ya jinai za Wazayuni wanaokalia ardhi zao kwa mabavu ni gaidi? Je, misaada ya kibinadamu kwa taifa hili na kulisaidia litatue matatizo yake ni kuusaidia ugaidi? Viongozi wa ubeberu unaotumia mabavu duniani hata hawahurumii thamani za kibinadamu. Wanadai etu hatua za kijinai za utawala katili na wa kigaidi wa Israel ni "kujilinda", lakini wakati huo huo wanautuhumu muqawama wa Palestina unaotetea uhuru, usalama na haki yake ya kujitawala kuwa ni "ugaidi"!

Suala jingine ambalo ni muhimu na linalopasa kuzingatiwa katika barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wanachuo wa Marekani ni sisitizo lake kuhusu njia iliyoko mbele ya matukio ya Asia Magharibi hususan Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Amesema katika barua hiyo kwamba: "Ninataka kuwahakikishia kuwa hali sasa inaendelea kubadilika. Hatima tofauti kabisa inalisubiri eneo nyeti la Asia Magharibi. Dhamiri nyingi zimeamka kote duniani na ukweli unaendelea kufichuka. Mrengo wa Muqawama nao umepata nguvu na utaendelea kupata mguvu zaidi. Historia pia inaendelea kubadilika."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amewataka wanachuo wa Marekani wanaotetea Palestina waendelee kuwa na subira na kupambana na mwishoni mwa barua yake akawaomba na kuwanasihi wapate kusoma na kukijua kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

Tags