Jun 27, 2024 02:59 UTC
  • Afisa wa Marekani aliyejiuzulu: Wanajeshi wa Marekani wanashiriki katika vita vya Israel huko Gaza

Afisa aliyejiuzulu kutoka Shirika la Ujasusi la Ulinzi la Marekani, Meja Harrison Mann, amesema kuwa vita vilivyoanzishwa na Israel katika Ukanda wa Gaza havingeweza kuendelea hadi leo bila msaada usio na kikomo wa Marekani, akisisitiza kwamba wanajeshi wa Marekani wanapigana katika kuilinda Israel.

Mann alikuwa akifanya kazi kama Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Shirika la Ujasusi la Ulinzi, na aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu Novemba mwaka jana baada ya kuthibitisha kwamba, mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yanalenga kuangamiza kabisa kizazi cha Wapalestina, na ni mauaji ya kimbari.

Afisa huyo wa Marekani aliyejiuzulu amesema - katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar- kwamba maofisa wengi na wafanyakazi wa taasisi hiyo ya ujasusi ya Marekani wana hisia sawa na iliyomfanya yeye ajiuzulu, lakini amesisitiza kwamba utawala wa Rais wa Marekani, Joe Biden, "hauna nia ya kusitisha msaada usio na masharti wala mpaka wa serikali ya Washinton kwa Israel."

Mann amesema: "Nilihisi kuwa kila siku ninapokwenda ofisini kwangu ninachangia katika mauaji ya Wapalestina, jambo ambalo lilinifanya nijiuzulu."

Maelfu ya watoto wa Palestina wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza

Ameeleza kuwa alikuwa akifanya kazi katika ofisi ambayo ni sehemu ya msaada wa kijasusi wa Marekani kwa Israel, na kwamba alihofia majibu ya wenzake katika jeshi na shirika hilo la ujasusi iwapo atawasilisha ombi la kujiuzulu, lakini anasisitiza kuwa alishangazwa na msimamo wao kwa sababu wengi walimuelewa na kumuunga mkono. 

Afisa huyo aliyejiuzulu wa Shirika la Ujasusi la Ulinzi la Marekani, Meja Harrison Mann, amesisitiza kwamba wengi katika taasisi ya ujasusi na jeshi la Marekani huwasiliana naye kwa ushauri, kwa sababu "wanahisi kama anavyohisi yeye kuhusu vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza, ambavyo havingeweza kuendelea bila msaada wa kijeshi wa Washington."

Tags