Jun 29, 2024 12:55 UTC
  • Iran yatoa onyo kali kuhusu vitisho vya Israel dhidi ya Lebanon

Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametahadharisha dhidi ya jaribio la utawala wa Kizayuni wa Israel la kupanua wigo wa vita na jinai katika maeneo mengine kwa lengo la kufidia kushindwa kwake katika Ukanda wa Gaza.

Katika mazungumzo yake ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal Bin Farhan, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Ali Bagheri Kani ameashiria jinai za kinyama zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na kusema kuwa vitisho vya utawala huo dhidi ya Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, ni muendelezo wa jinai za utawala huo katili dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Ali Bagheri Kani ameongeza kwa kusema kwamba utawala wa Kizayuni unajaribu kufidia kushindwa huko Gaza kwa kupanua wigo wa vita na uhalifu katika maeneo mengine.

Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa: Ni lazima kwa nchi za Kiislamu kutumia uwezo wao wote kusimamisha jinai, vitisho na hujuma za Wazayuni huko Gaza na maeneo mengine haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Faisal bin Farhan, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia ameeleza wasiwasi wake juu ya kushadidi mivutano kati ya utawala wa Kizayuni na Lebanon na kutoa wito wa kufanyika juhudi za kupunguza wigo wa vita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amesema mashauriano kati ya nchi hizo mbili kando ya mkutano wa 19 wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jukwaa la Majadiliano ya Ushirikiano wa Asia mjini Tehran yamekuwa na mafanikio na kusisitiza kuwa mchakato wa uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia umeimarika vya kutosha.

Tags