Jun 30, 2024 02:15 UTC
  • Mji wa Kanyabayonga DRC watekwa na waasi wa M23

Mji wa kimkakati wa Kanyabayonga, wa kaskazini mwa mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umetekwa na waasi wa M23.

Ripoti zinaeleza kuwa, mji huo umeangukia mikononi mwa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda baada ya mapigano na jeshi la Kongo.

"Wapiganaji wa M23 ndio wanaingia katikati mwa mji wa Kanyabayonga, nimewaona kwa macho yangu," mkazi mmoja kwa sharti la kutotajwa jina alisema. Taarifa iliyothibitishwa na mashirika ya kiraia katika eneo la Lubero.

Kundi la waasi la M23 ambalo linadaiwa kuwa na uhusiano na Rwanda lilitangaza pia mwezi uliopita wa Mei kwamba, limeuteka mji wa Rubaya ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao ni maarufu kwa madini muhimu yanayotumika katika utengenezaji wa simu za kisasa za mkononi.

Mapigano yamepamba moto katika miezi ya hivi karibuni kati ya waasi wa M23 na vikosi vya jeshi la Kongo, wakati Umoja wa Mataifa umeanza  kuwaondoa askari wake wa kulinda amani katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Mapigano makali kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Duru mbalimbali katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini zimeripoti kuhusiana na wimbi hilo jipya la wakimbizi.

Mwezi Januari mwaka huu Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendelezo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC dhidi ya waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.