Jul 01, 2024 02:20 UTC
  • Matokeo mabaya ya mauaji ya kikatili yanayofanywa na Wazayuni kwa wanawake huko Gaza

Miezi 9 imepita tangu utawala wa Kizayuni uanzishe mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Matabaka yote ya watu wa Ukanda wa Gaza yameathiriwa na jinai hizo za utawala wa Kizayuni wanazozifanya kila siku katika eneo hilo, lakini bila shaka, wanawake na watoto ndio wahanga wakubwa wa jinai hizo ambazo zimekuwa na taathira mbaya kwao kwa njia tofauti, na uharibifu huo ni suala ambalo Umoja wa Mataifa pia umekiri kuwa hauvumiliki na ni wa kinyama kwa watu hao.

Ukosefu wa usalama wa chakula ni moja ya matokeo ya mauaji ya kimbari ya Wazayuni kwa wanawake wa Ukanda wa Gaza.

 

Hali mbaya ya wanawake 60,000 wajawazito huko Ukanda wa Gaza

Katika ripoti yake mpya, Umoja wa Mataifa umeashiria hali mbaya ya wanawake huko Gaza na kutangaza kwamba; kwa uchahche wanawake 557,000 katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, jambo ambalo lina madhara ya kutisha kwao.

|Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa; hali mbaya ya ukosefu wa chakula huko Gaza inawalazimisha wanawake wengi kuacha wao na badala yake kuwapa watoto wao chakula.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uhaba wa chakula na utapiamlo mkubwa unaenea huko Gaza, na wanawake 7 kati ya 10 walioshiriki katika uchunguzi huo katika Ukanda wa Gaza walisema kuwa walipungua uzito sana katika mwezi uliopita, na zaidi ya nusu yao kuwa na kizunguzungu mara kwa mara.

Fauka ya hayo, uhaba wa chakula uliotwisha watoto na kuuawa shahidi wanaume iliwalazimu wanawake huko Gaza kuchukua jukumu la kutunza familia.

Kwa hakika, wanawake wa Gaza sio tu wanakabiliwa na mgogoro wa njaa, lakini wanapaswa kutoa chakula kidogo wanachopata kwa watoto wao ili waweze kuishi.

 Ripoti ya Umoja wa Mataifa pia inasema wakati wa migogoro mikali katika Ukanda wa Gaza, mzigo mkubwa unawekwa kwa wanawake, upatikanaji wao wa huduma wanazohitaji ni mdogo sana, na afya zao na usalama wa chakula uko hatarini.

Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni wa watu katika Ukanda wa Gaza, uhaba wa chakula umekuwa na athari mbaya kwa wanawake wa Ukanda wa Gaza.

Jambo lingine ni kwamba uhaba wa chakula ni mgumu na mkali zaidi kwa wajawazito kwa sababu husababisha afya zao pamoja na watoto na vichanga vyao kukabiliwa na hatari kubwa zaidi.

Na katika ripoti ya Umoja wa Mataifa pia inaeleza kuwa asilimia 76 ya wanawake wajawazito katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa damu, na asilimia 99 kati yao wanakabiliwa na changamoto nyingi katika upatikanaji wa bidhaa za chakula na virutubisho muhimu, jambo ambalo linahatarisha afya ya mama na watoto.

 

Njaa; Bomu la kimya kimya la utawala wa Kizayuni huko Gaza

Pia asilimia 99 ya akina mama wanaonyonyesha hawawezi kutoa maziwa ya kutosha kwa watoto wao, jambo ambalo linahatarisha ukuaji na afya ya watoto. Hii ni katika hali ambayo, vikosi vya Israel viliharibu kliniki kubwa zaidi ya uzazi katika Ukanda wa Gaza, ambayo inaripotiwa kuhifadhi vijusi 3,000.

Mbali na visa vilivyotajwa, wanawake wa Ukanda wa Gaza wamekuwa wakikabiliwa na shinikizo kubwa la kiakili na kihisia kutokana na kupoteza waume na watoto wao.

Sio miili yao tu, bali hata roho zao zimeteseka sana kutokana na huzuni na kupoteza wapendwa wao.

Hata hivyo hadi hivi sasa jumuiya ya kimataifa haijaweza kusimamisha jinai hizo kutokana na uungaji mkono wa kina wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na madola yote ya kibeberu na vibaraka wao kwa jinai hizo wanazofanya Wazayuni huko Palestina kwa watu madhulumu wasio na hatia.

Tags