Jul 01, 2024 10:56 UTC
  • Maseneta wa Kenya wamgomea Rais Ruto mpango wa kupunguza matumizi ya serikali

Rais William Ruto wa Kenya anakabiliwa na changamoto kubwa katika juhudi zake za kupunguza matumizi ya serikali ili kuziba pengo la bajeti la shilingi bilioni 346 huku maseneta wakiapa kukataa kupunguzwa kwa pesa za mgao wa kaunti.

Ni baada ya maseneta wa Kenya kumuonya Rais Willian Ruto asiingilie mgao wa shilingi bilioni 400.1 wa mapato uliotengewa kaunti 47, kama sehemu ya hatua zake za kupunguza matumizi.

Kiongozi wa Wachache katika Seneti ya Kenya, Ledama Olekina, ametaja tangazo la Rais Ruto la kupunguza matumizi kuwa ni ‘upumbavu,’ akiashiria sehemu ya 5 ya Sheria ya Mgao wa Mapato.

Seneta huyo wa Narok amesema, serikali ya kitaifa ndiyo inayopaswa kubeba upungufu wowote wa mapato na wala sio serikali za kaunti.

Olekina amemlaumu Rais William Ruto kwa kutaka kuchukua kazi ya Bunge ya kutunga sheria.

Wiki iliyopita Rais wa Kenya alitangaza kwamba pendekezo la kupunguza matumizi litatekelezwa kwa usawa na serikali za kitaifa na zile za kaunti.

Rais William Ruto

Haya yalijiri baada ya kiongozi wa Kenya kukataa kuidhinisha Muswada tata wa Fedha wa 2024 ambao ungefanya serikali ya kitaifa kuongeza mapato ya ndani kwa Sh. bilioni 346.