Jul 02, 2024 07:08 UTC
  • Kamanda Hajizadeh: Muqawama wa Palestina lazima utapata ushindi Gaza

Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hakuna chembe ya shaka kuwa muqawama wa Palestina utapata ushindi wa 'kishindo' mkabala wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh amenukuliwa akisema hayo na Press TV na kueleza kuwa, mrengo wa muqawama wa Palestina uko imara zaidi kuliko ulivyokuwa huko nyuma, na bila shaka utapata ushindi mkubwa dhidi ya Wazayuni huko Gaza.

Ameeleza bayana kuwa, mrengo wa muqawama huko Palestina si tu utabadilisha mlingano wa nguvu katika eneo la Asia Magharibi, lakini pia utabadilisha historia ya dunia.

Brigedia Jenerali Hajizadeh ameongeza kuwa, Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ilikuwa hatua ya mabadiliko makubwa katika historia ya Palestina na kwa muelekeo wa uwepo haramu wa utawala wa Kizayuni.

Kadhalika amesema maadui wanafahamu vyema uwezo mkubwa wa Iran na irada ya taifa hili la Kiislamu ya kuzima tishio lolote dhidi yake; hivyo maadui hawapaswi kuthubutu kuchukua hatua yoyote ya kuijaribu nchi hii.

Kamanda Hajizadeh amebainisha kuwa, utayarifu wa kulihami taifa la Iran hivi sasa upo katika kiwango cha juu zaidi katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Brigedia Jenerali Hajizadeh amesisitiza kuwa, Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya Iran ya Aprili 13 mwaka huu ilitokomeza na kufuta uwezo hewa na bandia wa kuzuia hujuma na mashambulio wa utawala wa Kizayuni.

Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la SEPAH ameongeza kwa kusema: Tunatumai fursa ya kufanya Operesheni ya Ahadi ya Kweli 2 itawadia.

Tags