Zambia kujinaisha matumizi ya sarafu ya dola
(last modified Wed, 03 Jul 2024 06:43:46 GMT )
Jul 03, 2024 06:43 UTC
  • Zambia kujinaisha matumizi ya sarafu ya dola

Benki Kuu ya Zambia imeandaa rasimu ya kanuni mpya zinazokusudia kuzuia matumizi ya sarafu za kigeni hususan dola ya Marekani katika miamala ya biashara ya ndani ya nchi.

Muswada huo unakusudia kuimarisha matumizi ya sarafu ya kitaifa ya kwacha na kuhimiza watu kutumia sarafu hiyo katika miamala na shughuli zote za sasa za bidhaa na huduma.

Iwapo muswada huo utapasishwa na kuanza kutekelezwa, watakaopatikana wakitumia sarafu za kigeni katika miamala ya ndani ya nchi watakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 10 jela au kutozwa faini kubwa.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Zambia, Francis Chipimo, hivi karibuni alisema kuwa, utegemezi na matumizi ya dola katika miamala ya ndani yana tatathira hasi na za muda mrefu kwa uchumi wa nchi; na kwamba kuachana na dola kutasaidia kuleta uwino katika kuhakikisha kuwa sarafu hiyo sio chaguo pekee linalotumika katika miamala ya kibiashara na mabadilishano ya kiuchumi ndani na nje ya nchi.

Serikali nyingi duniani zimefikia uamuzi wa kimkakati wa kujiweka mbali na sarafu ya dola ya Marekani ili kupunguza athari tarajiwa na madhara yanayoweza kutokea siku zijazo na kuathiri chumi za nchi zao.

Sarafu ya dola ya US inazidi kuporomoka kote duniani

Mwezi uliopita pia, Benki Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitoa agizo la kupunguza matumizi ya dola ya Marekani katika miamala ya bidhaa na huduma mbalimbali nchini humo. Aidha Mei mwaka huu, nchi wanachama wa kundi la BRICS la nchi zinazoinukia kiuchumi zilitangaza kufuatilia juhudi za kutupilia mbali sarafu ya dola ya Marekani katika miamala ya kibiashara na kiuchumi.

Moja ya nyenzo kuu za Marekani kwa ajili ya kutawala uchumi wa kimataifa na kuimarisha misingi ya uongozi wa Washington duniani ni sarafu ya nchi hiyo ya dola, ambayo imekuwa na inaendelea kutumika mara nyingi katika vita vya kiuchumi dhidi ya nchi ambazo haziko pamoja na Marekani kisiasa na kimisimamo.