Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran: Sarafu ya dola tumeiondoa katika miamala ya Iran na Russia
(last modified Sat, 13 Jul 2024 12:04:46 GMT )
Jul 13, 2024 12:04 UTC

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa miamala yote ya kibiashara kati ya Iran na Russia itafanyika bila ya kutumika sarafu ya dola.

Muhammad Baqer Qalibaf ameashiria uhusiano mkubwa wa nchi mbili za Iran na Russia na kusema nchi hizi zitaendesha biashara kati yazo bila ya kutumia dola ili kukabiliana na hatua za upande mmoja za Marekani. 

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran na Russia zina maslahi ya pamoja na pia adui wa pamoja na zimefikia makubaliano ya muda mrefu ya pamoja kwa ajili ya kushirikiana pande mbili katika nyanja za kijamii, kiutamaduni, kisiasa , kiusala na kiulinzi. 

Qalibaf ameeleza haya katika mahojiano na televisheni ya Russia Today. 

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amelitaja kundi la BRICS kuwa fursa muhimu kwa ajili ya nchi mbili za Iran na Russia kwa ajili ya kukuza ushirikiano wa pande mbili. 

Mkutano wa 10 wa Mabunge ya kundi la BRICS ulifanyika siku ya Alkhamisi huko St. Petersburg Russia kwa kuhudhuriwa na maspika wa mabunge ya nchi wanachama akiwemo Muhammad Baqer Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge). 

Kundi la kimataifa la BRICS liliasiwa na nchi tano zinazoibukia kiuchumi duniani ambazo ni Brazil, Russia, China, India na Afrika. Kundi hilo kwa kuwa na zaidi ya asilimia 30 ya eneo la dunia, nusu ya idadi ya watu duniani na nguvu ya kiuchumi ya zaidi ya asilimia 30  lina uwezo wa juu wa kuathiri uchumi wa dunia na lina umuhimu mkubwa katika ushirikiano wa kikanda. 

Nchi waasisi wa kundi la BRICS 

Nchi sita yaani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Argentina, Saudi Arabia, ,Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Ethiopia na Misri zimekuwa wanachama kamili wa BRICS tangu Januari mwaka huu.