Jibu la Russia kwa vitisho vya Trump dhidi ya BRICS
(last modified Tue, 11 Feb 2025 02:44:06 GMT )
Feb 11, 2025 02:44 UTC
  • Jibu la Russia kwa vitisho vya Trump dhidi ya BRICS

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa taarifa kuhusiana na tishio la Rais Donald Trump wa Marekani la kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za BRICS iwapo dola itafutwa katika mabadilishano ya kibiashara ya nchi hizo, na kusisitiza kuwa ushirikiano wa nchi wanachama wa BRICS unalenga kuimarisha uwezo wa kijamii, kiuchumi na kibinadamu wa nchi hizo.

Rais huyo mwenye utata mwingi wa Marekani, alitangaza Januari 30 kwamba Marekani itatoza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa kutoka nchi za BRICS ikiwa kundi hilo litatumia sarafu nyingine isiyokuwa dola katika biashara zake za kimataifa. Amesisitiza kuwa Marekani haitaruhusu dola kutelekezwa katika biashara ya kimataifa na kuonya kuwa nchi zitakazofanya hivyo zitakabiliwa na hatua kali za kibiashara kutoka Marekani. Kwa vitisho hivyo, Trump anajaribu kuzuia kuporomoka kwa udhibiti wa dola duniani kwa kuzitishia nchi ambazo tayari zimedhurika kutokana na satwa ya dola katika biashara na fedha za kimataifa na vilevile siasa za Marekani za kuitumia kama chombo cha kuadhibu na kuzikandamiza nchi nyingine.

Katika kujibu tishio la Trump, Dmitry Peskov, Msemaji wa Kremlin, ameashiria matamshi ya Rais Vladimir Putin wa Russia, ambaye awali alisema kuwa hakuna mipango yoyote ya kuunda sarafu ya pamoja katika kundi la BRICS, na kwamba limeazimia kuunda majukwaa mapya ya uwekezaji ambayo yataruhusu uwekezaji wa pamoja katika nchi za upande wa tatu. Desemba 2024, na katika kukabiliana na tishio la Trump la kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za BRICS, Putin alibainisha kuwa kutokana na vitendo vya Wademocrat, dola haina tena nguvu iliyokuwa nayo miaka minne iliyopita wakati wa urais wa kwanza wa Trump.

Sarafu ya BRICS

Mwishoni mwa mwezi Januari, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisisitiza kwamba kauli za Trump kuhusu kuwatoza ushuru mkubwa wanachama wa BRICS na kujiondoa katika baadhi ya mikataba ya kimataifa zinaonyesha mbinu zinazotumiwa na Washington kudhamini maslahi yake ulimwenguni. Alikumbusha kwamba maslahi ya Marekani daima yamekuwa yakilindwa kwa msingi wa kutaka kuifanya Marekani ionekane kuwa bora kuliko washindani wake wa kimataifa.

Matumizi mabaya ya Marekani ya dola kama chombo cha kuzikandamiza nchi nyingine daima yamekuwa yakilalamikiwa na mfumo wa sasa wa kifedha wa kimataifa kuliko jambo jingine lolote. Ingawa dola bado ndiyo sarafu kubwa zaidi ya akiba duniani, hatua ya Marekani ya kuitumia kama silaha ya kudhamini malengo yake duniani imezichochea nchi nyingi kuwekeza katika sarafu mbadala. Kutokana na Washington kutumia dola kama chombo cha kuziwekea mashinikizo nchi nyingine sambamba na vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi pinzani imezipelekea nchi hizo kuamua kutumia sarafu za kitaifa katika miamala yao ya kifedha na kibiashara.

Mwaka 2009, mataifa yenye nguvu na uchumi unaoibuka duniani yalijaribu kuanzisha umoja wa kisiasa na kiuchumi bila kuyashirikisha madola ya Magharibi, ambao uliitwa BRICS. Zikiwa katika kilele cha kundi la BRICS, China na Russia zinataka kukomesha utawala wa dola na uwezo wa kiuchumi wa nchi za Magharibi katika uhusiano wa kibiashara. Russia, ikiwa mwanachama muhimu wa kundi la BRICS, pamoja na wanachama wengine, kama vile Brazil, India, China, na Afrika Kusini, na baadaye Iran, Ethiopia, Indonesia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri, zinataka kutumia sarafu zao za kitaifa katika shughuli zote za kimataifa.

Nchi wanachama wa BRICS zina sababu nyingi za kutumia sarafu zao za kitaifa katika mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara na pia kuunda sarafu mpya ya BRICS. Sarafu ya BRICS ni sarafu ya kawaida ambayo ilizinduliwa na Rais Vladimir Putin wa Russia wakati wa mkutano wa kilele wa BRICS huko Kazan mnamo Oktoba 2024. Katika mkutano huo, Putin alizindua noti ya "Fedha Moja" mbele ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo. Wanachama wa BRICS walizindua jukwaa la BRICSPay katika mkutano huo na kusema kuwa linaweza kuwa na manufaa mengi kama vile kuondoa dola, kuwezesha biashara kati ya wanachama na kupunguza athari za vikwazo vya nchi za Magharibi. Sarafu hii imeundwa ili kupunguza kutegemea dola ya Marekani na kuunda mfumo huru wa kifedha. Changamoto za hivi karibuni za kifedha duniani na sera kali za kigeni za Marekani zimezifanya nchi za BRICS kufuata njia hii. Zinataka kuchukua hatua katika kulinda maslahi yao ya kiuchumi huku zikipunguza utegemezi wao wa kimataifa kwa dola ya Marekani na Euro.

kikao cha viongozi wa BRICS nchini Russia

Rais Putin amesema kuhusiana na suala hili kwamba: "Ushawishi wa dola katika ngazi ya kimataifa unapungua. Kwa kuzingatia kwamba hisa ya Marekani katika uchumi wa dunia inapungua, ni wazi kuwa ushawishi wa dola kwenye michakato ya uchumi wa dunia pia unapungua. Kwa kutokea hili, zana mpya zitaingia uwanjani na hakuna mtu anayeweza kuzuia utumiaji wa teknolojia na zana hizi mpya." Huku akiashria kuendelea kupungua kwa imani ya nchi za dunia kwa dola, Putin alisema: "Hata washirika wa Marekani yenyewe wanapunguza akiba ya dhahabu na fedha za kigeni kwa dola, kwa kadiri kwamba hisa ya dola katika akiba hii imepungua kwa asilimia 13 katika miaka 13 iliyopita."

Tishio la Trump dhidi ya wanachama wa BRICS kwa kutangaza ushuru wa asilimia 100 dhidi yao ikiwa watatumia sarafu ya BRICS linaonyesha hofu ya Washington kuhusu mabadiliko ya mwenendo kuu wa kifedha na kibiashara ulimwenguni.