WFP yatahadharisha kuhusu ongezeko la njaa duniani
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeeleza kuwa kupunguzwa kwa misaada ya nchi wafadhili kutazidisha mgogoro wa njaa unaozidi kuongezeka kote ulimwenguni, na kuonya kwamba zaidi ya watu milioni 300 watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka ujao.
"Uhaba wa chakula unatarajiwa kusalia katika viwango vya kutisha," shirika hilo limebainisha katika ripoti yake ya Global Outlook ya mwaka 2026 iliyotolewa jana Jumanne.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeeleza kuwa watu wanaokadiriwa milioni 318 watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka wa 2026, idadi inayotajwa kuwa sawa na kiwango cha "mgogoro" au kupindukia, na ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya watu walioathiriwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka 2019.
Shirika la WFP limesema kuwa linatarajia kulisha takriban watu milioni 110 ifikapo mwaka 2026, na kuacha idadi kubwa ya watu duniani wakihitaji msaada wa chakula.
Mpango wa Chakula Duniani umeongeza kuwa: Unakadiria kuwa unahitaji dola bilioni 13 mwaka 2026 ili kukabiliana na migogoro na gharama nyingine. Hii ni katika hali ambayo, utabiri wa sasa unaonyesha kuwa shirika la WFP linaweza kupokea karibu nusu ya kiasi hicho pekee.