Kwa nini sarafu ya dola si kimbilio salama tena duniani?
Baada ya miongo kadhaa ya juhudi za Marekani kudumisha utawala wa sarafu ya dola juu ya mfumo wa fedha duniani, hali ya dola sasa imefikia hatua mbaya.
Ingawa dola ya Marekani imekuwa ikijulikana kwa miongo kadhaa kama sarafu ya akiba ya kimataifa na mahali salama wakati wa migogoro ya kifedha, sasa kuna kila ishara kwamba nafasi hii inayumba na kulegalega.
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Chuo cha Brookings, msukosuko wa kisiasa na kifedha unaosababishwa na sera za ndani na nje za Marekani hasa katika kipindi cha urais wa Donald Trump, umezifanya nchi nyingi na wawekezaji wa kimataifa kuangalia upya imani yao kwa sarafu ya dola.
Chuo cha Brookings kimeonya kuwa, dola imefikia "hatua ya tahadhari" na wawekezaji wengi wa kigeni ambao hapo awali walizingatia sarafu ya dola na hati za dhama za Hazina ya Marekani kuwa mali salama zaidi, sasa wanatafakari upya.
Thamani ya dola imeshuka katika wiki za hivi karibuni, huku viwango vya riba nchini Marekani vikiongezeka suala ambalo katika hali ya kawaida ilipaswa kuimarisha sarafu ya dola. Tofauti hii imefasiriwa na wataalamu wa masuala ya fedha kama ishara ya masoko kutokuwa na imani na mustakabali wa uchumi wa Marekani.
Mfanano kati ya hali ya sasa ya Marekani na mgogoro wa kiuchumi nchini Uingereza mwaka 2022 umewatia wasiwasi wachambuzi wengi. Katika kipindi hicho pia, kupanda kwa deni la serikali ya Uingereza kulisababisha kushuka kwa kasi kwa thamani ya pauni na kupanda kwa hundi za dhamana. Hivi sasa hali kama hiyo inaelekea kutokea nchini Marekani.

Ripoti za kiuchumi zinaonyesha kuwa, vielelezo vya dola, ambavyo hupima nguvu ya sarafu hii dhidi ya sarafu sita, ikiwa ni pamoja na pauni, euro, na yen, vilishuka kwa asilimia 1.8 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.
Kwa mujibu wa tafiti, dola ya Marekani ilifanya vibaya zaidi katika kipindi cha miezi 6 ya kwanza ya mwaka huu kwa mara ya kwanza tangu 1973, na sera za kiuchumi za Rais Trump wa Marekani zimewafanya wawekezaji duniani kote kuuza haraka dola zao, jambo ambalo limehatarisha sana nafasi ya dola.
Ijapokuwa wataalamu wengi wametahadharisha kwa muda mrefu kuhusu kushuka kwa thamani ya dola, lakini sasa imeshika kasi kutokana na sababu za kisiasa na maamuzi ya kiuchumi ya Rais wa sasa wa Marekani.
Katika uga wa kiuchumi, sababu ni pamoja na kuongezeka kwa deni la umma la Marekani, kutoaminiwa kwa sera za kiuchumi, sera za upanuzi wa fedha, kupungua kwa mahitaji ya dola duniani, kutokuwa na uhakika wa kisiasa nchini Marekani, mfumuko wa bei na kupungua kwa uwezo wa ununuzi wa ndani.
Moja ya sababu muhimu za kudorora kwa dola ni vita vya kibiashara ambavyo Donald Trump ameanza na nchi zote duniani. Kutozwa kwa ushuru mkubwa kumeongeza hofu na wasiwasi kwa wawekezaji, huku pia kukizisukuma nchi kushirikiana na washirika wengine.
Kwa upande mwingine, utawala wa Trump umetumia nguvu ya dola kama chombo cha shinikizo la kisiasa kwa njia isiyo ya kawaida. Katika suala hili, vikwazo vya kiuchumi vya Marekani vimechukua mwelekeo mpana.
Marekani, kwa kutumia nafasi ya dola katika mabadilishano ya kimataifa, imezishinikiza vikali nchi kama vile Iran, Russia na Venezuela kufuata sera inazotaka, na pia imetishia kuzitoza ushuru baadhi ya nchi zingine.
Kutumia sarafu ya dola kama wenzo wa kushinikiza mataifa mengine kumeyafanya mataifa mengi kusita kuunganisha akiba zao zote za fedha za kigeni na njia za malipo za kimataifa.
Kwa hivyo, nchi nyingi zinatafuta njia mbadala. Kwa mfano, China inahimiza sana matumizi ya Yuan katika miamala ya kibiashara ya nchi mbili. Russia pia imebadilisha sehemu kubwa ya akiba yake ya dola kuwa euro na dhahabu.
Kwa upande mwingine, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuunda miungano mipya ya kiuchumi kama vile BRICS pia ni hatua za kupunguza utegemezi kwa dola katika mfumo wa uchumi wa kimataifa. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia Sergei Lavrov alisema kuhusiana na hili: Jamii ya kimataifa imekuwa na mwelekeo zaidi wa kuunda mifumo huru isiyo na uhusiano na Magharibi na filihali maeneo ya Mashariki na Kusini mwa Ulimwengu yanaonekana kugeuka na kuwa nguvu kuu ya ukuaji wa uchumi wa kimataifa. Masoko ya fedha pia yanathibitisha mabadiliko haya.
Wachambuzi wengi sasa wanaamini kwamba, ikiwa hali ya sasa itaendelea, dola inaweza kuwa chanzo cha mgogoro badala ya kuwa kimbilio salama wakati wa shida. Hii haimaanishi kuangamia kwa dola mara moja, lakini inaashiria kupoteza sarafu hii mashuhuri nafasi yake ya zamani katika uchumi wa dunia.
Kwa ujumla, tunachoshuhudia sasa ni dalili za mgogoro mkubwa. Mgogoro huu ni ishara ya kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na imani duniani na utungaji sera za kiuchumi na kimataifa za Marekani.
Inaonekana kwamba jibu la swali, "Je, dola bado ni kimbilio duniani?" kila siku linakaribia kuwa "hapana".