Mamilioni ya wananchi wa Uingereza wapiga kura katika uchaguzi mkuu
Wananchi wa Uingereza Alkhamisi leo wanapiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kukirejesha madarakani chama kikuu cha upinzani cha Labour, na kumaliza takribani muongo mmoja na nusu wa utawala wa chama cha Conservative.
Huu ni uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu Boris Johnson aliposhinda kwa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2019. Uchaguzi hu unafanyika baada ya Waziri Mkuu Rishi Sunak kuchukua hatua ya kushangaza ya kuitisha uchaguzi huo miezi sita mapema kuliko inavyotakiwa.
Upigaji kura ulianza tangu saa moja kamili asubuhi kwa saa za Uingereza kwenye zaidi ya vituo 40,000 vya kupigia kura nchini kote. Rishi Sunak alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza waliojitokeza kupiga kura katika jimbo lake la Richmond na Northallerton huko Yorkshire, kaskazini mwa England, akiwa ameongozana na mkewe Akshata Murty.
Baada ya miaka 14 madarakani chini ya mawaziri wakuu watano ndani ya kipindi cha miaka minane, chama cha Sunak cha Conservative kinatarajiwa kushindwa na chama cha Labour kinachoongozwa na Keir Starmer, chenye kufuata siasa za mrengo wa kushoto.
Viongozi wa vyama walitoa wito wao wa mwisho kwa wapiga kura baada ya kuzunguka nchi yote tangu uchaguzi ulipotangazwa. Waziri Mkuu Sunak alisema, siku ya Alhamisi inawakilisha wakati muhimu kwa mustakabali wa nchi, akidai kuwa chama cha Labour kitatumia nguvu zake zisizoweza kudhibitiwa kuongeza kodi ikiwa kitapata wingi wa kura.
Kwa upande wake Starmer amesema Uingereza haiwezi kumudu miaka mitano zaidi chini ya chama cha Conservative, akiongeza kubainisha kuwa Uingereza inaweza kuanza ukurasa mpya chini ya chama chake.