Human Rights Watch: Vikosi vya Ethiopia vimetenda jinai za kivita Amhara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113686-human_rights_watch_vikosi_vya_ethiopia_vimetenda_jinai_za_kivita_amhara
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, vikosi vya Ethiopia vimefanya jinai za kivita katika eneo la Amhara.
(last modified 2024-07-04T08:41:59+00:00 )
Jul 04, 2024 08:41 UTC
  • Human Rights Watch: Vikosi vya Ethiopia vimetenda jinai za kivita Amhara

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, vikosi vya Ethiopia vimefanya jinai za kivita katika eneo la Amhara.

Ripoti ya shirika hilo inaeleza kuwa, vikosi vya Ethiopia vimetekeleza mashambulizi makubwa kama "jinai za kivita" dhidi ya sekta ya afya katika eneo la Amhara.

Ripoti ya Human Rights Watch yenye kurasa 66 ambayo iliwahoji  watu takriabn 58 wakiwemo waathirika na mashuhuda, imesajili visa vya mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya serikali na wanamgambo wa Fano dhidi ya wahudumu wa sekta ya afya, vituo vya afya pamoja na miundombinu ya usafirishaji katika miji takriban 13.

Sehemu ya ripoti hiyo ya Human Rights Watch inaeleza jinsi askari walivyowapiga, kuwakamata kiholela wahudumu wa afya kwa kosa la kuwapa huduma majeruhi na wagonjwa ikiwa ni pamoja na wapiganaji wanaodaiwa kuwa wa Fano.

 

Aidha ripoti hiyo imeongeza kuwa vikosi hivyo vilishambulia magari ya wagonjwa kinyume na sheria na kuzuia hospitali kutoa huduma.

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limesema kuwa, sheria ya kimataifa ya kibinaadamu inatoa ulinzi kwa miundombinu katika sekta ya afya, wahudumu, wagonjwa, lakini sheria hiyo imekiukwa kwa kiwango kikubwa wakati wa makabiliano na kuleta hofu miongoni mwa waathirika katika mzozo huo.

Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika Laetitia Bader amesema kwamba vikosi vya serikali ya Ethiopia viliendesha operesheni zake kwa "kupuuza maisha ya raia" kwa kushambulia miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na vituo vya afya.