Rais wa China amuonya Trump kuhusu Taiwan; usifanye makosa
Rais wa China ameonya katika mazungumzo yake na mwenzake wa Marekani, Donald Trump huko Beijing kuhusu hatua zozote za Washington katika Kisiwa cha Taiwan, akisema: Kosa lolote linaweza kusababisha mzozo kati ya nchi hizo mbili.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jana Alkhamisi mjini Beijing, Rais Xi Jinping wa China alionya kwamba mwenendo wowote usiofaa wa Washington kuhusu suala la Kisiwa cha Taiwan unaweza kuzitumbukiza nchi hizo mbili katika makabaliano hata ya vita na kudhoofisha uhusiano wa China na Marekani kwa njia hatari. Xi Jinping amesisitiza kuwa: Suala la kujitawala Taiwan haliuendani na amani kisiwani humo.
Beijing inaitambua Taiwan kama sehemu isiyoweza kutenganishwa ya Jamhuri ya Watu wa China na inalitaja suala la kufuata "kanuni ya China Moja" kama sharti muhimu kwa nchi zinazotaka kuanzisha au kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na China.
Kabla ya hapo China kwa mara nyingine tena ilitangaza upinzani wake mkali dhidi ya hatua ya Marekani ya kuzidisha himaya na uungaji mkono wake wa kijeshi kwa Taiwan sambamba na ziara ya Rais Trump mjini Beijing.
Maafisa wa China wameendelea kusisitiza kuwa Taiwan inasalia kuwa suala la ndani na wamelaani ushirikiano wote wa kijeshi kati ya kisiwa hicho na Washington, ambayo haina uhusiano rasmi wa kidiplomasia na kisiwa hicho.