Washington Katika Mkwamo
https://parstoday.ir/sw/news/event-i138366-washington_katika_mkwamo
Jarida la Marekani la The Atlantic hivi karibuni lilichapisha ripoti iliyochunguza kwa mapana na marefu vipengele vya makabiliano ya kijeshi kati ya Marekani na Iran pamoja na athari zake. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, sera na hatua za Washington hadi sasa hazijawa na matokeo yaliyotarajiwa, na zimeisababishia Marekani vizuizi na changamoto kali.
(last modified 2026-05-15T07:59:58+00:00 )
May 15, 2026 07:40 UTC
  • Donald Trump na mkwamo wa Washington
    Donald Trump na mkwamo wa Washington

Jarida la Marekani la The Atlantic hivi karibuni lilichapisha ripoti iliyochunguza kwa mapana na marefu vipengele vya makabiliano ya kijeshi kati ya Marekani na Iran pamoja na athari zake. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, sera na hatua za Washington hadi sasa hazijawa na matokeo yaliyotarajiwa, na zimeisababishia Marekani vizuizi na changamoto kali.

Katika historia ya mahusiano ya kimataifa, athari za kila vita na mapigano huwa haziishii kwenye mipaka ya uwanja wa mapigano tu; lakini husambaa pia kwenye uga wa kiuchumi, kisiasa na kijiopolitiki. Marekani leo hii, inakabiliwa na mgogoro ambao wigo wake ni mpana zaidi kulinganisha na tajiriba ilizopitia nchi hiyo katika kadhia ya Pearl Harbor, Vietnam au Afghanistan. Jarida la The Atlantic limetahadharisha katika ripoti yake mpya kwamba endapo Marekani itashindwa katika makabiliano na Iran si tu kushindwa huko hakutaweza kufidika, lakini kutapindua na kubadilisha pia mizani ya mlingano wa nguvu duniani.

Uzoefu na tajiriba iliyopata Marekani huko nyuma unaonyesha kuwa, kushindwa kwake, hata kama kuliendelea kwa muda, kuliweza kufidika na hakukuwa na taathira ya kudumu kwa nafasi yake kimataifa. Lakini wataalamu kama Robert Kagan wanaamini kwamba makabiliano ya sasa na Iran ni tofauti kabisa. Kwa Muqawama ilioonyesha dhidi ya mashambulizi ya kijeshi na mashinikizo ya kiuchumi, Iran imeifanya Washington ikabiliwe na mgogoro ambao haijawahi kuushuhudia, ambao athari zake zinaweza kusambaa ulimwengu mzima.

Kushinda au kushindwa Marekani katika mgogoro huu sio tu kutabadilisha nafasi ya nchi hiyo, lakini kutapindua pia mizani ya mlingano wa kikanda na kimataifa. Kushindwa Washington kunaweza kuimarisha nafasi ya China na Russia zikiwa ni washirika wa Iran, kupunguza itibari ya Marekani mbele ya washirika wake wa Ulaya na Asia, na kuongeza kasi ya mchakato wa kuelekea kwenye mfumo wa dunia wa baada ya enzi za Marekani.

Wapenzi wasikilizaji, katika makala hii ya wiki, na kama tulivyotangulia kueleza tunataka kuangazia ripoti iliyochapishwa na jarida la Marekani la The Atlantic, ambayo ndani yake imeakisi uchambuzi wa Robert Kagan, mmoja wa shakhsia wahafidhina mamboleo mwenye ushawishi mkubwa katika mkondo huo wa kisiasa nchini Marekani. Ripoti hiyo inachunguza matokeo yanayoweza kushuhudiwa kutokana na makabiliano ya kijeshi kati ya Marekani na Iran, na kuweka wazi athari zake za kijeshi, kisiasa na kimataifa.

Katika andiko lake hilo, Kagan anasema, Rais Trump anazungumzia kuhusu nani anayeshikilia “karata ya turufu” mkononi mwake, lakini bado haijabainika kama anazo kweli karata zinazofaa kwa ajili ya kuchezea au la.

Mashambulizi ya siku 40 ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, yaliyohusisha mauaji ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa na kijeshi, hayajawa na mafanikio yoyote yanayoeleweka kwa Washington. Serikali ya Iran haijaanguka, wala haijaweza kulazimishwa iipatie Washington fursa za upendeleo inazotaka. Hali hii inaonyesha kiwango cha Muqawama na ungangari wa Iran ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha kuhimili mashambulizi ya kijeshi na mashinikizo ya kiuchumi; ambacho athari zake zinaweza kuvuka mipaka ya eneo la Asia Magharibi.

Kagan anasisitiza kuwa, Trump hakusitisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa sababu ya kuchoshwa nayo, lakini sababu ya kufanya hivyo ilikuwa ni kulengwa na Iran miundombinu muhimu ya nishati katika eneo. Anasema, mabadiliko muhimu sana yalitokea tarehe 18 Machi, ambapo baada ya utawala wa Kizayuni kushambulia viwanda vya gesi vya Iran vya Pars Kusini, vikosi vya ulinzi vya Iran viliilenga mitambo ya Ras Laffan nchini Qatar ambapo mjibizo alioonyesha Trump kwa shambulizi hilo ulikuwa ni kutangaza usitishaji vita pasi na kupata hata fursa ndogo kabisa ya upendeleo kutoka kwa Iran.

Kagan anaitakidi kuwa, kudhibiti Iran Mlango-Bahari wa Hormuz kunaipa uwezo wa kioperesheni unaozidi hata uwezo wa kinadharia wa nyuklia. Iran inaweza kudhibiti au kuzuia upitaji wa meli, kuweka ushuru, kulazimisha kutimiziwa na nchi zingine masharti yake ya kiuchumi na kisiasa, na kuathiri mwenendo wa mataifa madogo na makubwa katika eneo hilo.

Jarida la The Atlantic linaonya kuwa, hatua yoyote ile ghairi ya kusalimu amri Marekani itakuwa na hatari kubwa. Kujiingiza kwenye vita kamili vya nchi kavu na baharini kwa lengo la kuiangusha serikali ya Iran kunaweza kupelekea kupotea maisha ya wanajeshi pamoja na kuangamizwa meli za kivita, jambo ambalo linaongeza uwezekano wa kushindwa Marekani. Kwa sababu hiyo, kulegeza msimamo au kujiondoa linaweza likawa chaguo lenye madhara madogo zaidi kwa Washington.

Matokeo na athari za kushindwa Marekani zitavuka mipaka ya kikanda. Itibari ya Washington mbele ya washirika wake wa Ulaya na Asia itapungua, na washirika wa Iran, wakiwemo China na Russia, wanaweza kushadidisha hatua zao za mashambulizi. Mwenendo huo utaharakisha na kuongeza kasi ya kuibuka dunia ya baada ya enzi za Marekani na kupungua ushawishi wa Washington katika milingano ya kimataifa.

Kwa kuendelea kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, Iran itageuka kuwa mdau mkuu wa kimkakati katika eneo. Kagan anaendelea kusema, nchi hiyo inaweza kuathiri sera za nishati duniani, kuweka mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi kwa nchi za Ghuba ya Uajemi, na hata kuzuia hatua za kichochezi za Israel. Hali hiyo inadhihirisha mabadiliko ya mizani ya nguvu katika eneo pamoja na kupungua ushawishi wa Marekani.

Mchambuzi huyo mhafidhina mamboleo anasisitiza kuwa, kushindwa Marekani si jambo tu linaloweza kutokea, lakini kunaweza pia kuibua mlolongo mpana wa athari. Mgogoro huu unatilia shaka uwezo wa Marekani wa kutekeleza operesheni kubwa za kijeshi katika siku za usoni, na unawafanya washirika wake barani Asia na Ulaya wawe na shaka juu ya nguvu na uwezo wa Washington.

Kwa kumalizia, jarida la The Atlantic linafikia hitimisho kwamba, makabiliano haya, tofauti na madai ya baadhi ya waungaji mkono wa vita, hayaonyeshi nguvu za Marekani, bali yanadhihirisha udhaifu na kutoweza Washington kukamilisha kile ilichokianzisha. Matokeo ya kushindwa huko, iwe ni katika kiwango cha kikanda au kimataifa, yatabadilisha muundo wa nguvu pamoja na sera za kiuchumi na kijiopolitiki, na yataharakisha mchakato wa kufikia kwenye dunia ya baada ya enzi za ubabe wa Marekani.

Kinachopatikana kutokana na uchambuzi wa ripoti ya jarida la The Atlantic na tathmini ya Robert Kagan ni kuonyesha kwamba makabiliano kati ya Marekani na Iran yanaelekea mbali zaidi na kuvuka mpaka wa mgogoro wa kikanda. Kushindwa Washington sio tu kutatilia shaka nguvu za kijeshi za nchi hiyo, lakini pia kutabadilisha mizani ya mlingano wa kijiopolitiki na kiuchumi katika Asia Magharibi na duniani kwa ujumla.

Udhibiti wa Iran kwa Mlango-Bahari wa Hormuz umeunda wenzo wa kiutendaji wenye uzito na umuhimu mkubwa, unaozidi hata uwezo wa kinadharia wa nyuklia. Tehran inaweza kuziweka njia muhimu za kupitishia mafuta na gesi chini ya satua na udhibiti wake, na kuathiri moja kwa moja mwenendo wa kiuchumi na kisiasa wa nchi zingine.

Matokeo ya kushindwa Marekani yatakwenda mbali zaidi ya eneo; washirika wa nchi hiyo barani Ulaya na Asia wataanza kutilia shaka itibari ya Washington, huku China na Russia zikitarajiwa kuongeza hatua zao za ushawishi na mashambulizi ya kimkakati. Mwenendo huo utaharakisha mchakato wa kuelekea kwenye dunia ya baada ya enzi za Marekani na kupungua satua na ushawishi wa Washington katika milingano ya kimataifa.

Kwa kuendelea kuwa na uwezo wa kuudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, Iran itageuka kuwa mdau mkuu wa kimkakati katika eneo hilo na itaweza kuelekeza na kutekeleza sera za nishati, uchumi na siasa kwa manufaa yake. Nchi za Ghuba ya Uajemi na hata Israel zitakuwa chini ya mashinikizo ya kidiplomasia na kiuchumi; na kwa hali hiyo, hakutakuwa na uwezekano wa kurejea katika hali iliyokuwepo kabla ya mgogoro huo.

Mapitio ya ripoti ya jarida la Marekani la The Atlantic yanaonyesha kuwa, sera na hatua za kijeshi za Marekani katika kukabiliana na Iran hazijawa na matokeo yaliyotarajiwa, na badala yake zimeibua vizuizi na athari zisizotarajiwa kwa Washington. Ripoti hiyo inasisitiza kwamba hata baada ya mashambulizi makubwa, udhibiti wa maeneo muhimu ya kimkakati katika eneo ikiwemo Mlango-Bahari wa Hormuz ungali uko mikononi mwa Iran, na Marekani inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za kiutendaji na kijiopolitiki.

Ripoti hiyo inatahadharisha pia kwamba hatua yoyote mpya ya kijeshi au kiuchumi itakayochukuliwa bila ya kufanyiwa tathmini ya kina juu ya hatari zake inaweza kusababisha athari zenye wigo mpana zaidi kwa Washington na washirika wake katika ngazi ya kimataifa.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya Makala ya Wiki kwa juma hili umemalizika. Hivyo Sina budi kukomea hapa. Nakushukuruni kwa kuwa nami kuanzia awali hadi tamati ya mazungumzo yetu na nakuageni huku nikikutakieni kheri na fanaka maishani …/