Araqchi katika mkutano wa BRICS New Delhi: Ushawishi wa Marekani unapungua
-
Abbas Araqchi katika mkutano wa BRICS, New Delhi India
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amesema kuwa wananchi wa Iran "wamesimama kidete na kwa fahari " dhidi ya machafuko ya kutisha, na kamwe hawatasalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani nchi ambayo ushawishi wake duniani unazidi kupungua.
Araqchi ameeleza haya wakati akihutubia mkutano wa siku mbili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Wanachama wa Kundi la BRICS mjini New Delhi siku ya Alhamisi, ulioandaliwa na Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Inapasa kufahamika wazi kwamba, Iran haiwezi kuvunjika na kusambaratika bali inaibuka na nguvu na kushikamana zaidi pale inapokabiliwa na mashinikizo.
Amesema, Iran iko tayari kuendeleza mapambano kwa kustafidi na suhula zake zote ili kupigania uhuru, mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yake yote na ipo tayari kufuata na kutetea diplomasia.
"Sayyid Abbas Araqchi ameongeza kuwa, Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi ya kinyama na yaliyo kinyume cha sheria dhidi ya Iran katika muda wa chini ya mwaka mmoja kwa kutegemea madai ya uwongo ambayo ni kinyume na ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na hata Shirika la Ujasusi la Marekani lenyewe CIA.