Jul 02, 2024 14:53 UTC
  • Maandamano ya vijana Kenya yaendelea, waandamanaji wamtaka Rais Ruto aondoke madarakani

Vijana wa Kenya, wengi wao wakiwa Generation Z, wamerejea barabarani katika maandamano yaliyopewa jina la #OccupyEverywhere dhidi ya utawala wa Rais William Ruto.

Maandamano hayo yanayopinga serikali yametikisa miji mikubwa ya Kenya, huku vijana waandamanaji wakieleza kutoridhishwa na serikali ya muungano wa Kenya Kwanza.

Maandamano hayo ya kila wiki ambayo sasa yanaathiri uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki yameendelea licha ya Rais William Ruto kuinua juu tawi la mzeituni kwa vijana wanaoshiriki kwa wingi katika maandamano hayo. Jumapili iliyopita, Rais Ruto alisema yuko tayari kwa mazungumzo ya ana kwa ana au ya mtandaoni na vijana hao.

Maandamano hayo sasa yameendelea licha ya kiongozi huyo kukubali shinikizo la waandamanaji na kukataa kutia saini Muswada wa Fedha wa 2024 uliopasishwa na Bunge, kuwa sheria.

Waandamanaji wanamtaka Rais Ruto aondoke madarakani.

Polisi Jijini Nairobi wamelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kukabiliana na waandamanaji katika ghasia zilizopeleke kufungwa biashara nyingi katika mji huo. 

Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika miji mingine mikubwa ya Kenya kama Mombasa na Kisumu. 

Mashirika ya kiraia yametangaza kuwa, watu 53 wameshauawa kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano hayo huku jiji la Nairobi likiripoti vifo 30.

Waandamanaji hao wa Kenya sasa wanamtaka Rais wa nchi hiyo, William Ruto, ajiuzulu licha ya uamuzi wake wa kuweka kando Muswada wa fedha wa 2024 uliokuwa umedhamiria kuongeza ushuru ili kusaidia kupunguza mzigo wa madeni nchini humo.

Tags