Mapigano yaendelea Sudan huku juhudi za kuwakutanisha majenerali hasimu zikifeli
Mapigano kati ya jeshi na kikosi cha msaada wa haraka yameshadidi tena nchini Sudan huku juhudi za kuwakutanisha majerali hasimu nchini huumo zikigonga mwamba.
Taarifa zaidi zinasema, kwa upande mmoja, vikosi vya usaidizi wa haraka vimeteka maeneo ya jimbo la Senar, na kwa upande mwingine, jeshi limeteka tena eneo la Al-Doha huko Omdurman.
Mapigano nchini Sudan yanaripotiwa kushadidi katika hali ambayo, mkutano wa kisiasa kuhusu Sudan unatarajiwa kufanyika Jumamosi ya keshokutwa Julai 6 huko Cairo Misri. Wakati huo huo, Yasser Atta, Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Suudan amekanusha habari ya kuwepo mpango wa mkutano kati ya Rais wa Baraza Kuu la Utawala nchini Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, na kiongozi kundi la waasi wa RSF Hamdan Dagalo Hemedti, akipinga ripoti zinazodai kwamba mkutano huo utafanyika hivi karibuni nchini Uganda.
Yasser al-Atta amesema kuwa mazungumzo yoyote na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yatakayopelekea kumalizika vita lazima yatanguliwe na kutimizwa masharti kadhaa.
Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.
Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan kutokana na vita vya kuwania madaraka kati ya majenerali wawili waitifaki wa zamani, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan na Luteni Jenerali Hamdan Dagalo.