Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran awaonya maadui, mkijaribu mtashindwa tena
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, amezionya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu kuanzisha tena hatua mpya za kijeshi dhidi ya Iran, akisema kuwa makabiliano ya awali yalishindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa, na kwamba jaribio lolote la baadaye litakuwa na matokeo yaleyale.
Mwanadiplomasia huyo mkuu alitoa kauli hizo pembeni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa BRICS uliofanyika New Delhi siku ya Alhamisi, akijibu vitisho vilivyotolewa na maafisa mbalimbali wa Marekani na Israel.
Araghchi amesema: “Tumezoea vitisho hivi. Kwa muda mrefu wamekuwa wakirudia vitisho vyao kwa namna na sura tofauti. Lakini wao wenyewe pia wanajua kwamba hawakupata chochote, wala hawatapata chochote kupitia vitisho hivyo au hata kupitia vita walivyoanzisha.”
Ameongeza kuwa: “Natumai wataachana na lugha ya vitisho na kuelekea kwenye mantiki, ingawa matumaini ni madogo kwamba watarejea kwenye busara. Lakini wanapaswa kufahamu kwamba suluhisho la masuala mbalimbali halipatikani vitani, kwa sababu hawatapata matokeo yoyote kupitia njia hiyo.”
Araghchi pia amesema kuwa nafasi ya Iran katika eneo la Magharibi mwa Asia imeimarika kufuatia ushindi dhidi ya washambuliaji. Ameongeza kuwa: “Sasa, mataifa yote yanatambua kwamba Jamhuri ya Kiislamu ndiyo iliyoshinda katika vita hivi na ilifanikiwa kuwazuia maadui wake kufikia malengo yao huku ikilazimisha matakwa yake yenyewe.”
Kwa mujibu wa Araghchi, mijadala katika mkutano wa BRICS imeonyesha kuwepo tathmini mpya ya hali ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Magharibi mwa Asia baada ya vita.
Amekumbusha kwamba, kwa hatua ya kujibu mashambulizi dhidi yake, Iran ililenga “ngome za Marekani pekee kwenye ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.”
Waziri wa mambo ya nje pia ametoa wito wa kuwa na mtazamo tofauti kuhusu usalama wa eneo la Asia Magharibi.
Aidha amesema amemshauri mwakilishi wa Umoja wa Falme za Kiarabu katika kikao cha BRICS kwamba utawala wa Kizayuni na Marekani haziwezi kuwadhaminia usalama, kama ambavyo sasa wameona athari za kuhifadhi kambi za kijeshi za Marekani.
Araghchi aidha amesisitiza umuhimu wa uhusiano mwema kati ya nchi jirani na ushirikiano wa majirani katika masuala ya usalama badala ya kuwategemea wageni.