UN yaonya kuwa mamilioni wanakabiliwa na njaa DRC kutokana na vita
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138370-un_yaonya_kuwa_mamilioni_wanakabiliwa_na_njaa_drc_kutokana_na_vita
Onyo kali limetolewa na Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa njaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaoendelea kuwa mbaya zaidi, huku zaidi ya watu milioni 26.5 wakihangaika kupata mahitaji yao ya msingi ya chakula kila siku.
(last modified 2026-05-15T09:42:22+00:00 )
May 15, 2026 09:40 UTC
  • Njaa DRC
    Njaa DRC

Onyo kali limetolewa na Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa njaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaoendelea kuwa mbaya zaidi, huku zaidi ya watu milioni 26.5 wakihangaika kupata mahitaji yao ya msingi ya chakula kila siku.

Katika taarifa ya pamoja, ya mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo FAO na la Mpango wa Chakula Duniani WFP yamesema karibu mtu mmoja kati ya wanne nchini humo anakabiliwa na viwango vya njaa vya dharura, huku zaidi ya watu milioni 3.6 wakiwa tayari katika hali mbaya inayotishia maisha yao.

Mashirika hayo yameeleza hali hiyo kuwa moja ya migogoro mikubwa na mibaya zaidi ya njaa duniani. Yamesema mapigano yanayoendelea katika majimbo ya mashariki mwa DRC kama Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri na Tanganyika yamesababisha familia kuhama makazi yao, kuharibu maisha yao na kuvuruga shughuli za kilimo.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, zaidi ya watu milioni 7.8 wameyakimbia makazi yao ndani ya nchi, wengi wao wakipoteza mashamba, mifugo na vyanzo vya mapato.

Hali ya kibinadamu nchini humo imeendelea kuzorota kutokana na kupanda kwa bei za chakula, kuvurugika kwa usafirishaji wa bidhaa pamoja na milipuko ya mara kwa mara ya magonjwa ya kipindupindu, surua na Mpox.

Wahudumu wa misaada wameonya kuwa jamii ambazo tayari ni dhaifu zinakaribia maafa makubwa zaidi huku ukosefu wa usalama ukizuia upatikanaji wa misaada kwa wahitaji wengi.

Mashirika ya misaada sasa yanatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa haraka ili kuzuia mgogoro huo kuzidi kuwa mbaya zaidi. Yamesisitiza kuwa msaada wa dharura wa chakula pekee hautoshi bila uwekezaji wa muda mrefu katika kilimo, maisha ya wananchi na mifumo imara ya chakula.