Satelaiti tatu za Iran kurushwa katika anga za mbali karibuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138368-satelaiti_tatu_za_iran_kurushwa_katika_anga_za_mbali_karibuni
Shirika la Anga za Mbali la Iran (ISA) limetangaza kwamba satelaiti tatu zilizotengenezwa ndani ya nchi zimeingia katika hatua ya mwisho ya majaribio, ishara kwamba mpango wa anga wa kiraia wa nchi hii unastawi kwa kasi licha ya mashinikizo kutoka nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni.
(last modified 2026-05-15T09:38:24+00:00 )
May 15, 2026 09:33 UTC
  • Satelaiti ya Zafar ya Iran iliyotengenezwa ndani ya nchi
    Satelaiti ya Zafar ya Iran iliyotengenezwa ndani ya nchi

Shirika la Anga za Mbali la Iran (ISA) limetangaza kwamba satelaiti tatu zilizotengenezwa ndani ya nchi zimeingia katika hatua ya mwisho ya majaribio, ishara kwamba mpango wa anga wa kiraia wa nchi hii unastawi kwa kasi licha ya mashinikizo kutoka nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni.

Hassan Salariyeh, Shirika la Anga za Mbali la Iran, amesema satelaiti zilizoboreshwa za Pars-1, Pars-2, pamoja na Rad-1 yenye rada, zinakamilisha majaribio ya kabla ya kurushwa katika anga za mbali

Ameongeza kuwa sekta hiyo imepata “mafanikio ya thamani” kwa msaada wa serikali na Wizara ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano.

Aidha, amebainisha kuwa miundombinu inayofaa imejengwa kote nchini, uwezo wa tasnia ya anga za mbali umegawanywa katika maeneo mbalimbali ya Iran.

Salariyeh amesisitiza kuwa tasnia hii, inayotegemea maarifa, inachochewa na utaalamu wa vijana na wasomi wa Kiirani, akibainisha kuwa Shirika la Anga za Mbali la Iran imeharakisha juhudi za kukamilisha satelaiti mpya.

Maendeleo yanayoendelea katika mpango wa satelaiti wa Iran yanajiri wakati miundombinu kadhaa ya kiraia ya anga na vituo vyao ililengwa wakati wa vita vya siku 40 vya uchokozi vilivyoanzishwa Februari 28 bila sababu na tawala dhalimu za Marekani na Israeli.

Vituo kadhaa vinavyohusiana na anga vililengwa kwa makusudi, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Anga za Mbali, Taasisi ya Utafiti wa Mifumo ya Satelaiti, Taasisi ya Utafiti wa Usafiri wa Juu wa Anga za Mbali, Taasisi ya Utafiti wa Uendeshaaji wa Roketi za Anga za Mbali, pamoja na Kituo cha Anga cha Mahdasht, na pia miundombinu ya ardhini ya udhibiti wa satelaiti katika Kituo cha Khayyam.

Katika barua iliyopelekwa Umoja wa Mataifa, Iran ililaani mashambulizi hayo kama vitendo vya ugaidi wa kiserikali.