Jul 02, 2024 04:13 UTC
  • Bagheri: Waliomuunga mkono Saddam katika jinai ya Sardasht wanaunga mkono jinai za Wazayuni Ukanda wa Gaza

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika siku ya kumbukumbu ya mashambulizi ya silaha za kemikali katika mji wa Sardasht nchini Iran kwamba: Wale waliounga mkono jinai za utawala wa Saddam Hussein dhidi ya watu wa Sardasht nchini Iran hivi sasa wanaunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Gaza.

Shughuli ya kumbukumbu ya kushambuliwa mji wa Sardasht nchini Iran, hujuma ambayo ilifanywa na utawala wa Baath wa Saddam na Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Silaha za Kemikali na Vijidudu ilifanyika jana Jumatatu katika Idara ya Masuala ya Kisiasa na Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ikihudhuriwa na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje, mabalozi na wawakilishi wa nchi za nje na baadhi ya maveterani waliojeruhiwa katika hujuma hiyo ya silaha za kemikali.  

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri Kani 

Mwanzoni mwa shughuli hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali alisisitiza katika ujumbe wake aliotoa kwa njia ya mtandao juu ya ulazima wa kuangamizwa maghala ya silaha za kemikali. Fernando Arias alisema: "Nchi zote lazima ziheshimu mkataba wa marufuku ya matumizi ya silaha za kemikali. 

Ali Bagheri Kani Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliashiria vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel vya kutumia silaha za kemikali dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kusema: Ukweli mchungu na tishio la sasa ni kuendelea jinai za Israel huko Gaza, ambazo jamii ya kimataifa inapaswa kuzikomesha.  

Bagheri Kani ameashiria upuuzaji na kutochukua hatua zozote jamii ya kimataifa khususan nchi za Magharibi mkabala wa jinai za Israel dhidi ya watu wa Gaza - suala lililoandaa uwanja wa kuendelezwa jinai hizo - na kukumbusha kuwa, Wairani  elfu kumi waliuawa shahidi kwa silaha za maangamizi makubwa ya utawala wa Saddam, na nchi za Magharibi zilikuwa na nafasi kuu katika kumpatia Saddam silaha hizo. 

Utawala wa Baath wa Iraq Juni 28 mwaka 1987 ulitumia mabomu ya kemikali kushambulia maeneo manne ya kaunti ya Sardasht katika mkoa wa Azerbaijan Magharibi, unaopatikana kaskazini magharibi mwa nchi. Raia 119 wa eneo hulo waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 8,000 walidhurika kwa gesi ya sumu na kupata maradhi ya aina mbalimbali.

Tags