Jul 02, 2024 11:47 UTC
  • Jeshi la Yemen lashambulia meli 4 zenye mfungamano na Israel, Marekani, Uingereza

Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimetekeleza oparesheni kadhaa za kijeshi na kuzipiga kwa makombora meli nne katika Bahari Nyekundu, Arabian Sea, Mediterania na Hindi katika kuonyesha mshikamano na raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa jeshi la Yemen Meja Jenerali Yahya Saree amesema vikosi vya Yemen vimezishambulia meli hizo nne zenye mfungamano na Marekani, Uingereza na utawala wa Israel kwa makombora ya Criuse na kuzilenga bila kukosea. 

Meja Jenerali, Yahya Saree

Jeshi la Yemen limetaja meli hizo zilizozipigwa kuwa ni meli ya mafuta ya Marekani ya Delonix, meli ya uingereza ya Anvil Point na ile ya Lucky Sailor.

Jeshi la Yemen limekuwa likizishambulia kwa droni na makombora meli zote zinazomilikiwa na utawala wa Israel, zenye bendera ya utawala wa Kizayuni, au zile zinazoelekea katika bandari za utawala huo haramu katika kuonyesha mshikamano na raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza wanaokabiliwa na mauaji ya kimbari na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Israel tangu Oktoba mwaka jana. 

Wapalestina zaidi ya elfu 37 wameuawa shahidi wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, na  wengine zaidi ya 86,300 kujeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza Oktoba mwaka jana.