Putin asifu uhusiano unaokua kwa kasi kati ya Russia na Uturuki
(last modified Thu, 04 Jul 2024 02:25:48 GMT )
Jul 04, 2024 02:25 UTC
  • Putin asifu uhusiano unaokua kwa kasi kati ya Russia na Uturuki

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa uhusiano kati ya nchi yake na Uturuki unakuwa kwa kasi licha ya changamoto zilizopo za kimataifa.

Rais wa Russia amesema kuwa mauzo ya biashara kati ya Russia na Uturuki yako katika kiwango cha juu cha dola bilioni 55 licha ya kupungua kidogo kwa mauzo ya biashara kati ya nchi mbili katika miezi michache iliyopita.

Rais Vladimir Putin alisema haya jana katika mazungumzo na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, pambizoni mwa Mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan. 

Mkutano wa Jumuiya ya Shanghai mjini Astana 

Katika mazungumzo hayo, Putin alisisitiza kuwa miradi mikubwa ya pamoja inaendelea kutekelezwa kama iliyopangwa.

Kwa upande wake Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki amekariri mwaliko wake kwa Rais wa Russia kwa ajili ya kuitembelea tena Uturuki siku zijazo. 

Ziara kadhaa zilizopangwa za Putin nchini Uturuki ziliahirishwa katika miezi ya hivi karibuni kwa sababu kadhaa kama vile uchaguzi uliofanyika katika nchi zote mbili mapema mwaka huu.