Jul 02, 2024 12:33 UTC
  • Lavrov kuendesha mjadala wa Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya Kati

Russia ambayo inashikilia uwenyekiti wa kiduri wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Julai imetangaza kuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov ndiye atakayesimamia vikao kadhaa vya mikutano ya baraza hilo mwezi huu, ikiwa ni pamoja na mjadala kuhusu hali ya mambo ya Mashariki ya Kati.

Shirika la habari la Tass limeripoti kuwa, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeeleza kuwa matukio matatu makuu yanapangwa kujadiliwa katika kipindi hiki ambapo Russia ni Mwenyekiti wa kiduru wa Baraza la Usalama la UN. Matukio hayo ni pamoaj na mijadala miwili ya wazi ukiwemo ule utakaoangazia ushirikiano wa nchi mbalimbali duniani ili kuasisi muundo wa dunia wa haki, demokrasia na endelevu zaidi.  

Mjadala uliopangwa kufanyika tarehe 16 mwezi huu utaongozwa na Sergei Lavrov; na unategemewa kuwa mwendelezo wa majadiliano yaliyofanywa chini ya uenyekiti wa Russia Aprili mwaka jana. Katika wiki ya tatu ya mwezi huu wa Julai kutafanyika pia matukio mawili makubwa ikiwemo mjadala wa wazi kuhusu Mashariki ya Kati ambapo Tor Wennesland Mratibu Maalumu wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati pia atazungumza. 

Vassily Nebenzia Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa hali ya mambo huko Palestina pia itajadiliwa. 

 

Tags