Jul 01, 2024 12:39 UTC
  • Joe Biden
    Joe Biden

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na mtandao wa CBS wa Marekani ambao matokeo yake yalichapishwa jana Jumapili, umeonyesha kuwa takriban robo tatu ya wapiga kura waliojiandikisha nchini Marekani wanaamini kuwa Rais Joe Biden hana afya ya kiakili inayomfanya astahiki kuchaguliwa tena kuongoza nchi katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Uchunguzi huo wa maoni ambayo ilifanywa kwa muda wa siku mbili zilizopita umebaini kuwa asilimia hiyo imepanda kutoka 65 mwanzoni mwa mwezi huu hadi 72% baada ya mdahalo wa karibuni wa Joe Biden na mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump, ambao umemsababishia wimbi kubwa la ukosoaji.

Kwa upande mwingine, nusu ya wapiga kura wa Marekani waliojiandikisha wanaamini kwamba Trump ana afya ya akili inayomwezesha kutawala nchi kuanzia Januari 20 ijayo ikiwa atashinda dhidi ya Biden.

Kwa upande mwingine, viongozi wa chama cha Democratic mapema leo wametangaza uungaji mkono wao kwa Biden (umri wa miaka 81) licha ya utendaji wake duni wakati wa mdahalo wake na Trump. Wakati huo huo Ikulu ya White House imekanusha ripoti kwamba Rais Joe Biden amekutana na familia yake kutathmini mustakabali wa kugombea kwake.

Uungaji mkono huo wa chama cha Democratic kwa Biden unakuja kufuatia utendaji wake dhaifu Alhamisi iliyopita katika mdahalo na Donald Trump, ambapo alionekana kusitasita na kudumaa mara kwa mara, na pia kuparaganyika kimawazo, jambo lililoibua wasiwasi zaidi kuhusu uzee na umri wake mkubwa.

Joe Biden

Katika muktadha huo, gazeti la New York Times limekuwa gazeti la kwanza la Marekani kumtaka rais aliyeko madarakani, Joe Biden, kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais wa 2024 kufuatia utendaji dhaifu katika mdahalo dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump siku chache zilizopita.

Katika duru ya kwanza ya midahalo ya kabla ya uchaguzi ujao wa rais unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, wateule hao watarajiwa kuwakilisha vyama viwili vikuu vya Marekani katika uchaguzi huo, walibishana kuhusu uchumi wa Marekani, sera ya kigeni, COVID, uavyaji mimba na uhamiaji, huku wakirushiana matusi ya nguoni, na kutaja majina watu wa familia zao, masuala ya maadili, na hata kila mmoja wao kumpa changamoto mpinzani wake kwenye mechi ya golfu.