Jul 02, 2024 02:36 UTC
  • Kuondolewa Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya magaidi ya Arab League, matunda ya kikanda ya Kimbunga cha  Al-Aqsa

Baada ya miaka 8 kupita, hatimaye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeliondoa jina la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwenye orodha yake ya kigaidi.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ina ushawishi mkubwa katika eneo hili na ina nafasi muhimu katika mlingano wa nguvu wa ukanda huu. 

Ingawa Hizbullah ya Lebanon ina utambulisho wa Kiarabu, lakini baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo hili mara nyingi zinaweka sera za kuifanya Hizbullah ni adui yao. Mfano wa wazi ni yale yaliiyotokea mwaka wa 2016, wakati Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilipoiingiza Hizbullah ya Lebanon katika orodha yake ya magaidi.

Kuondolewa  Hizbullah katika orodha ya magaidi ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni mafanikio kikanda ya operesheni ya kimbunga cha  Al-Aqsa 

Tarehe 11 Machi 2016, Arab League iliitaja Hizbullah ya Lebanon kuwa eti ni "taasisi ya kigaidi" na kuitaka "kukomesha kile ilichodai kueneza misimamo mikali na kimadhehebu, kujiepusha kuingilia masuala ya ndani ya nchi na isijihusishe kwa namna yoyote katika masuala ya eneo hili. 

Tangazo hilo la Arab League dhidi ya harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon lilitolewa muda mfupi baada ya nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kudai kuwa eti Hizbullah ya Lebanon ni taasisi kigaidi mnamo Machi 2, 2016.

Kwa hivyo basi, hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ilisababishwa na mambo mawili. Jambo la kwanza lilikuwa ni hatua ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ya kuitangaza Hizbullah kuwa ni taasisi ya kigaidi, na sababu nyingine ni mvutano uliokuwepo katika uhusiano wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Lakini baada ya kupita miaka 8, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeiondoa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwenye orodha yake ya kigaidi.

Njama za kuidhibiti Hizbullah ya Lebanon zinaendelea kufeli

Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Hussam Zaki alitangaza siku ya Jumapili tarehe 29 Juni, 2024, kwamba Jumuiya hiyo haiiangalii tena Hizbulah kwa jicho la taasisi ya kigaidi.

Matamshi hayo ya Hussam Zaki yalitangazwa siku moja baada ya kumalizika safari yake huko Beirut, na alisema kupitia kituo cha televisheni cha Al-Qahira cha Misri kwamba, huko nyuma maamuzi ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yalikuwa ni kuitangaza Hizbullah ya Lebanon kuwa ni taasisi ya kigaidi, lakini hivi sasa nchi hizo zimekubaliana kutotumia jina la kigaidi kwa Hizbullah, na zimefungua milango ya kushirikiana na harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu. 

Siku ya Ijumaa, gazeti la Lebanon la Al-Akhbar liliripoti kwamba; Zaki alitembelea Beirut na kukutana na Mohammad Raad, mkuu wa kundi la waungaji mkono wa muqawama lenye mfungamano na harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Hayo yalikuwa ni mawasiliano ya kwanza kabisa kati ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Hizbullah ya Lebanon katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Kiujumla tunaweza kusema kuwa, uamuzi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wa kuiondoa Hizbullah ya Lebanon katika orodha yake ya magaidi umetokana na mambo kadhaa. Jambo la kwanza ni kubadilika kwa uhusiano wa baadhi ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia ulifufuliwa mwezi Machi 2023 wakati wa serikali ya 13 ya Iran iliyokuwa inaongozwa na Rais Ebrahim Raisi aliyekufa shahidi katika ajali ya helikopta, tarehe 19 Mei mwaka huu.

Sababu nyingine ni operesheni ya kimbunga cha al-Aqsa iliyoongozwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, dhidi ya utawala wa Kizayuni. Mara baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya Wapalestina hasa wa Ghaza hapo tarehe 7 Oktoba 2023, Hizbullah ya Lebanon nayo ilingia vitani kupambana na utawala wa Kizayuni na hadi hivi sasa inapambana na adui huyo katili kuwaunga mkono ndugu zao Wapalestina. 

Hizbullah ya Lebanon ina nafasi muhimu sana katika nyoyo za watu

Wataalamu wengi wa mambo wanasema kuwa, uamuzi huo mpya wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni ishara ya kuweko mabadiliko makubwa katika milinganyo ya kisiasa kwenye eneo hili baada ya operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa na kuongezeka umaarufu wa Hizbullah ya Lebanon miongoni mwa wananchi wa nchi za Kiarabu za eneo hili kutokana na uungaji mkono wa dhati wa harakati hiyo kwa ndugu zao Wapalestina.

Jambo la mwisho kuhusu uamuzi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, tunaweza kusema kuwa umetokana na mtazamo chanya wa viongozi wa nchi za Kiislamu kuhusu ulazima wa kukomeshwa jinai za Israel huko Ghaza na kupunguza mivutano na machafuko katika eneo hili.

Tags