Jun 30, 2024 06:56 UTC
  • Arab League yaiondoa Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetangaza habari ya kuiondoa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika orodha yake ya 'mashirika ya kigaidi'.

Kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar imemnukuu Hossam Zaki, Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu akisema kuwa, Arab League imeacha kuitambua Hizbullah kama shirika la kigaidi.

Amesema: Baada ya Hizbullah ya Lebanon kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Kizayuni wakati wa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, Arab League ilitangaza kuwa haiitazami tena harakati hiyo kama 'kundi la kigaidi'.

Zaki ameeleza bayana kuwa, katika maamuzi yake ya huko nyuma, Arab League iliitambua Hizbullah kama shirika la kigaidi kutokana na maazimio yaliyopasishwa na nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya Waarabu.

Kadhalika Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema masharti yaliyowekwa kwa ajili ya nchi wanachama wa Arab League kuanzisha uhusiano na Harakati ya Hizbullah yametimizwa.

Wanamuqawama wa Hizbullah ya Lebanon

Ikumbukwe kuwa, Machi 11 mwaka 2016, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliitaja Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuwa kundi la kigaidi. Uamuzi huo ulikosolewa vikali si tu na viongozi wa Lebanon, bali na mrengo wote wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi.

Lebanon na makundi ya muqawama yalieleza kuwa, Arab League inapaswa kufungamana na makubaliano ya Waarabu ambayo yalitofautisha baina ya muqawama na ugaidi.

Lebanon inasisitiza kuwa, muqawama na mapambano ya wananchi wa Lebanon ni kielelezo cha wazi cha "Haki ya Kisheria ya Kujihami"ambayo imeashiriwa katika kipengee cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, na ni haki ya kisheria ambayo imetumiwa na Lebanon kwa ajili ya kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi.

Tags