Jul 02, 2024 11:35 UTC
  • Kukosoa Umoja wa Mataifa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vyay walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu umekosolewa na Umoja wa Mataifa.

Ujenzi wa vitongoji vya walowezi ni moja ya jinai muhimu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Jinai hii ina umri wa miaka 76. Kwa maana kwamba, jinai hii imekuwa ikifanyika tangu kuasisiwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Sababu kuu ya kuendelezwa jinai hiyo kwa takriban miongo 8 ni kung'angania utawala wa Kizayuni kupanua ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu, na kubadilishwa muundo na utambulisho wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa kuwapa makazi raia wa Israel.

Ni kwa msingi huo, ndio maana jamii ya kimataifa imepinga mara kadhaa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Mwishoni mwa mwaka 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 na kutangaza kwa mara nyingine tena kwamba, ujenzi wowote unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria na kusisitiza juu ya ulazima wa kuhamishwa mara moja vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni vilivyojengwa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Utawala wa Kizayuni umekuwa ukikiuka mara kwa mara azimio hili na sio tu kwamba haujasimamisha ujenzi huo, bali umeongeza kasi yake.

Moja ya sababu kuu za ukiukwaji wa wazi wa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Uumoja wa Mataifa unaofanywa na  utawala wa Kizayuni ni sera za Marekani za kutoa himaya na uungaji mkono kwa  utawala huo ghasibu. Hadi sasa kwa uungaji mkono wa Marekani na kutumia kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa utawala wa Kizayuni umekuwa ukipuuza mara kwa mara matakwa ya pande mbalimbali ukiwemo Umoja wa Ulaya ya kutaka kuhitimisha sera zake za kujitanua pamoja na jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.

 

Kutotekelezwa maazimio hususan azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kunaupa kiburi utawala wa Kizayuni cha kuzidisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi na kuhujumu juhudi za kimataifa za kukomesha uvamizi huo na kupatikana amani. Ni kwa muktadha huo ndio maana licha ya upinzani wa kimataifa dhidi ya vitongoji vya walowezi na uvamizi wa utawala wa Kizayuni, katika miongo kadhaa iliyopita, utawala huo ghasibu umeongeza unyakuzi na uporaji zaidi wa ardhi za Wapalestina na badala yake kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ukiwemo mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.

Katika hatua ya karibuni kabisa, vyombo vya habari vya Kizayuni vimetangaza kuwa, Baraza la Mawaziri la Israel Alkhamisi iliyopita lilitangaza kuwawekea vikwazo viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Katika kukabiliana na ongezeko la kukubalika kwa zaidi ya nchi 140 kutokana na kutambuliwa taifa la Palestina, Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha wa utawala wa Kizayuni alipendekeza kuwekewa vikwazo maafisa wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina pamoja na kuhalalisha kujengwa kwa vitongoji vitano vya walowezi katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan. Tayari pendekezo hilo limekubaliwa.

Israel imekuwa ikibomoa nyumba za Wapalestina kwa visingizio mbalimbali

 

Kwa mujibu wa duru za Wazayuni, Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni pia limekubali kutangaza zabuni za ujenzi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanyika kikao cha Baraza Kuu la Mipango ili kuidhinisha mipango ya ujenzi wa maelfu ya nyumba za makazi ya walowezi wa Kizayuni.

Uamuzi huo umekabiliwa na upinzani mkali kieneo na kimataifa. Tor Vansland, mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya amani Asia Magharibi, ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: Tangazo la hivi karibuni la mmoja wa mawaziri wa baraza la usalama la utawala wa Israel kuhusu kuhalalisha kisheria upanuzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, unatia wasiwasi na kudhoofisha juhuudi za utatuzi wa mgogoro huo.

Tags