Benki ya Dunia yaidhinisha dola milioni 207.6 za kukabiliana na ukame Zambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113646-benki_ya_dunia_yaidhinisha_dola_milioni_207.6_za_kukabiliana_na_ukame_zambia
Benki ya Dunia imeidhinisha msaada wa dola milioni 207.6 wa kuisaidia serikali ya Zambia kukabiliana na ukame.
(last modified 2024-07-03T07:13:11+00:00 )
Jul 03, 2024 07:13 UTC
  • Benki ya Dunia yaidhinisha dola milioni 207.6 za kukabiliana na ukame Zambia

Benki ya Dunia imeidhinisha msaada wa dola milioni 207.6 wa kuisaidia serikali ya Zambia kukabiliana na ukame.

Pesa hizo ni ufadhili wa pili wa ziada kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa kijamii nchini Zambia. Pesa hizo zitazisaidia familia zipatazo milioni 1.6 katika wilaya 84 zilizoathiriwa na ukame nchini humo.

Situmbeko Musokotwane, Waziri wa Fedha na Mipango wa Zambia ameishukuru Benki ya Dunia kwa msaada huo akisema kuwa, utasaidia mpango wa serikali wa kukabiliana na ukame kwa kuongeza uhawilishaji fedha za kijamii ili kusaidia kukabiliana na nakisi za mara kwa mara za bajeti.

Kwa mujibu wa waziri huyo, hatua ya Benki ya Dunia ya kuidhinisha ufadhili huo wa pili wa ziada itaimarisha mipango iliyopo ya ulinzi wa kijamii na kupunguza athari mbaya za ukame ambazo zimeikumba Zambia ambayo tayari inateseka kwa uhaba wa rasilimali za ndani.

Mvua chache zilinyesha nchini Zambia katika msimu wa kilimo wa 2023/2024 na hivyo kusababisha ukame ambao umeathiri wilaya 84 kati ya 116 za nchi hiyo.

Hii ni kusema kuwa, Zambia, Malawi na Zimbabwe zote zimetangaza hali ya dharura na janga kwa sababu ya ukame, ambao umeathiri uzalishaji wa chakula na maisha ya mamilioni ya watu.

Miongoni mwa malengo ya msaada mpya wa Benki ya Dunia kwa Zambia ni kuisaidia serikali ya nchi hiyo kutoa malipo ya ziada ya pesa taslimu kwa kaya zilizoathirika.