Jul 03, 2024 07:21 UTC
  • Wapalestina 250,000 walazimika kuwa wakimbizi huko Khan Yunis

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza kuwa watu 250,000 wamelazimishwa na utawala wa Kizayuni kuyahama makazi yao katika mji wa Khan Yunis, na kuwa hakuna sehemu salama kwao katika eneo hilo.

Shirika la habari la Quds Feed lilitangaza jana Jumanne kwamba wakimbizi wa Kipalestina sasa wanaishi barabarani baada ya kufukuzwa kwenye mahema yao mashariki mwa Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa ripoti hii, maelfu ya wakimbizi wa Kipalestina waliondoka kwenye mahema yao jana usiku huko Khan Yunis, hasa katika maeneo ya mashariki, kufuatia amri ya jeshi la utawala unaoikalia kwa mabavu Quds ya kuhamwa maeneo hayo kwa madai kuwa ni hatari, ambapo sasa wanaishi barabarani.

Pia, hospitali pekee iliyoko Khan Yunis imehamisha wagonjwa wake, wakimbizi wa Kipalestina na vifaa vya matibabu.

Israel imeamuru kufukuzwa Wapalestina 250,000 kutoka kusini mwa Ukanda  Gaza

Wakati huo huo, utawala unaokalia Quds kwa mabavu (Israel) umekiri rasmi kuhusu kuuawa wanajeshi wake wanne katika muda wa saa 24 zilizopita huko Khan Yunis.

Shirika la habari la Palestina "Shahab" pia; limeripoti kuwa wanaharakati wa muqawama wa Brigedi ya Qassam wameua au kujeruhi wanajeshi kadhaa wa  utawala katili wa Israel katika makabiliano na askari wa jeshi la utawala huo wanaokwenda kwa miguu katika kitongoji cha Shujaiyeh mashariki mwa mji wa Gaza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, Wapalestina 38,000 wameuawa shahidi na zaidi ya 87,000 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7, 2023, mwaka jana.

Katika muda wa saa 24 zilizopita, jeshi la utawala wa Israel limefanya mauaji na jinai tatu za kutisha dhidi ya Wapalestina katika ukanda huo ambapo limeua shahidi Wapalestina 25 wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine 81 huko Khan Yunis.