Watu 25 wafa maji katika hamkani za kukimbia vita nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113720-watu_25_wafa_maji_katika_hamkani_za_kukimbia_vita_nchini_sudan
Takriban watu 25 wamekufa maji kusini mashariki mwa Sudan walipokuwa wakijaribu kukimbia mapigano ya uchu wa madaraka kati ya jeshi la Sudan SAF na Viikosi vya Msaada wa Haraka RSF.
(last modified 2024-07-05T06:49:58+00:00 )
Jul 05, 2024 06:49 UTC
  • Watu 25 wafa maji katika hamkani za kukimbia vita nchini Sudan

Takriban watu 25 wamekufa maji kusini mashariki mwa Sudan walipokuwa wakijaribu kukimbia mapigano ya uchu wa madaraka kati ya jeshi la Sudan SAF na Viikosi vya Msaada wa Haraka RSF.

Taarifa hiyo imetolewa na  kamati ya wanaharakati wanaounga mkono demokrasia nchini Sudan ambayo pia imesema: "Takriban watu 25, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo, wamekufa maji baada ya boti yao kuzama wakati walipokuwa wanavuka mto wa Blue Nile katika jimbo la Sennar la kusini mashariki la Sudan.

Kamati hiyo ni moja ya taasisi zilizokuwa zikiandaa maandamano ya mamia ya watu kote nchini Sudan kupigania demokrasia, na muda wote huu wa vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi, kamati hiyo iko mstari wa mbele kupigania amani na kukomeshwa mapigano kati ya jeshi SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF.

Wahanga wakuu wa vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan, ni raia wa kawaida

 

Sehemu moja ya taarifa ya kamati hiyo imesema: "Familia zote zilizopoteza maisha katika ajali hiyo zilikuwa ziko hamkani kukimbia mapigano makali katika ya wanajeshi hao huko Sennar."

Siku ya Jumamosi, RSF ilitangaza kuwa imeteka kambi ya kijeshi ya mji wa Sinja ambao ndiyo makao makuu ya jimbo la Sennar. Zaidi ya watu laki tano wamekimbilia huko kutafuta hifadhi kutokana na vita. Siku ya Jumatatu Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, takriban watu 55,000 wameukimbia mji wa Sinja pekee katika kipindi cha siku tatu zilizopita.

Wakuu wa jimbo jirani la Gedaref jana walisema kuwa wanakadiria kwamba, watu 120,000 wamekimbilia kwenye jimbo hilo. Waziri wa afya wa jimbo hilo Ahmed al-Amin Adam amesema kuwa wakimbizi 90,000 wamesajiliwa rasmi jimboni humo.