Hizbullah yashambulia Israel kwa makombora baada ya kamanda wake kuuawa
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeshambulia kwa mamia ya makombora kambi kadhaa za kijeshi za utawala wa Kizayuni Israel huko kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, kujibu chokochoko za jeshi hilo katili.
Hizbullah imesema katika taarifa kuwa, wanamapambano wa harakati hiyo ya muqawama jana Alkhamisi, walishambulia kwa makombora 200 kambi kadhaa za kijeshi na timu za lojistiki za Wazayuni, kaskazini mwa Palestiona inayokaliwa kwa mabavu.
Taarifa ya Hizbullah imeongeza kuwa, makombora yake yamelenga kwa usahihi shabaha zilizokusudiwa kwenye operesheni hiyo ya ulipizaji kisasi, na kulisababishia jeshi la Kizayuni hasara kubwa.
Baadhi ya vituo na kambi za kijeshi za Wazayuni zilizoshambuliwa jana Alkhamisi na wanamuqawama wa Hizbullah ni Kikosi cha 91 katika kambi ya Ayelet, Brigedi ya 7 katika kituo cha kijeshi cha Katsaviya, na makao makuu ya Batalioni ya Vifaru ya Brigedi ya 7 katika kambi ya Gamla.
Kadhalika Hizbullah ilishambulia makao makuu ya Divisheni ya 210 (Divisheni ya Golan) katika kambi ya Nafah na makao makuu ya wanajeshi waendao kwa miguu wa Divisheni ya 210 katika kituo cha Yarden. Aidha wamamuqawama wa Lebanon wamesambaratisha kikamilifu kwa kombora la Burkan kituo cha kijeshi cha Wazayuni cha al-Marj.
Harakati ya Hizbullah imesema imefanya operesheni hiyo kulipiza kisasi, baada ya Wazayuni maghasibu kumuua shahidi mmoja wa makamanda wa harakati hiyo hiyo ya muqawama, Mohamed Naim Nasser, katika shambulio la droni katika mji wa al-Housh eneo la Tyre, kusini mwa Lebanon.
Ikumbukwe kuwa, Hizbullah imekuwa ikifanya mashambulizi ya makombora, maroketi na droni karibu kila siku dhidi ya maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, ili kuonyesha mshikamano wao na Wapalestina wasio na ulinzi wa Gaza.