Askari wa SADC wahitimisha operesheni dhidi ya ugaidi kaskazini mwa Msumbiji
Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika nchini Msumbiji (SAMIM) kimetangaza kuwa, kimeamua kuondoka katika jimbo la Cabo Delgado la kaskazini mwa Msumbiji ikiwa ni kiashirio kwamba kikosi hicho kimefanikiwa kurejesha usalama na amani jimboni humo.
Sherehe za kutamatishwa kazi za kikosi cha SADC zimeongozwa na Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, Cristovao Chume na Mkuu wa kikosi hicho cha SADC, Mpho Molomo huko Pemba, makao makuu ya jimbo hilo la Cabo Delgado la kaskazini mwa Msumbiji.
Katika hotuba yake, waziri huyo aliishukuru SADC kwa kupelekea huko kikosi cha SAMIM na kuisaidia Msumbiji katika vita dhidi ya ugaidi.
Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji pia amesema kuwa, maficho ya magaidi yameharibiwa, shughuli za kiuchumi zimeanza tena, watu wanatembea kwa uhuru na wameanza kurudi polepole katika maeneo yao ya asili. Yote hayo ni ushahidi wa kuimarika usalama katika jimbo hilo.
Pamoja na hayo waziri huyo ameonya kuwa, licha ya kupatikana mafanikio hayo na kufikia hatua ya kuondoka kikosi cha SAMIM, lakini bado kuna harakati za kigaidi katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Cabo Delgado. Kwa sasa wanajeshi wa Msumbiji na Rwanda wanaendelea kupiga doria kwenye maeneo hayo.
Kikosi cha SADC kilipelekewa nchini Msumbiji mwezi Julai 2021 baada ya kutolewa idhini hiyo na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika. Hatua hiyo ya ushirikiano wa kikanda ilikuwa ni kuitikia ombi la serikali ya Msumbiji la kusaidiwa kupambana na magaidi ambao walikuwa wanahatarisha usalama wa ukanda huo mzima.