Jul 01, 2024 11:28 UTC
  • Mamia ya maafisa wa jeshi Israel wataka kuondoka jeshini, hawataki tena kushiriki katika vita vya Gaza

Televisheni ya Israel imetanagaza kuwa maafisa wapatao 900 wa vyeo tofauti wa jeshi wameomba kufutwa mikataba yao ya  kuhudumu jeshini, wakati maombi kama hayo hapo awalii hayakuzidi maafisa 150.

Awali gazeti la Israel la Haaretz liliripoti kwamba makumi ya wanajeshi wa akiba wametangaza kwamba hawatarejea katika utumishi wa kijeshi huko Gaza, hata kama wataadhibiwa.

Haya yanakuja baada ya vyombo vya habari vya Kiebrania kufichua kwamba mamia ya wanajeshi wa Israel wametorekea nje bila ya kuwafahamisha makamanda wao, huku utawala huo ukiwa katika vita vya Gaza ambavyo vimesababisha hasara kubwa kwa utawala huo kiuchumi na kijeshi. 

Wakati huo huo, tovuti ya Walla ya Israel imerupoti kuwa jeshi linakabiliwa na uhaba wa wanajeshi, na linataka kuunda kitengo kipya cha kutekeleza majukumu mbalimbali.

Siku chache zilizopita askari wa akiba wa Israel walitangaza kwamba hawatarejea katika utumishi wa jeshi katika Ukanda wa Gaza, hata kama wataadhibiwa, jambo ambalo linaonyesha ukweli halisi katika uwanja wa vita, na ni ushahidi kutoka kwa adui mwenyewe wa ufanisi wa wanamapambano wa Kipalestina.

Jeshi la Israel hoi

Gazeti la Haaretz liliripoti kuwa, makumi ya wanajeshi wa akiba wa Israel wametangaza kwamba hawatarejea tena katika utumishi wa jeshi katika Ukanda wa Gaza hata kama wataadhibiwa, huku vyombo vya habari vya Israel vikiripoti kuwa mamia ya wanajeshi wa akiba katika jeshi la utawala huo hukimbilia nje kila mwezi bila kuwajulisha makamanda wao.

Mtaalamu wa masuala ya kijeshi, Meja Jenerali mstaafu Wassef Erekat amesema kuwa, vyombo vya habari vya Kiebrania vimelifedhehesha jeshi la Israel baada ya kufichua kwamba mamia ya wanajeshi wametorekea nje bila ya kuwafahamisha makamanda wao, jambo ambalo linaashiria dosari katika udhibiti na mawasiliano ya kijeshi na tatizo la kimkakati ambalo haliwezi kupatiwa ufumbuzi.