Kuzidi kuwa mkubwa mzozo na mpasuko ndani ya utawala wa Kizayuni
Kuendelea vita katika Ukanda wa Ghaza na kushindwa utawala wa Kizayuni kupata mafanikio yoyote ya kijeshi sambamba na chokochoko zinazofanywa na Netanyahu katika mpaka wa Lebanon ni mambo ambayo yamezidisha mzozo na mpasuko katika safu za Wazayuni.
Wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel, wanaendelea kufanya maandamano makubwa yakiwemo yale ya Jumamosi ambayo yalifanyika kwenye miji na maeneo 80 yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni ili kumshinikiza waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ajiuzulu; yeye na genge lake la Kizayuni lenye misimamo mikali serikalini.
Yair Lapid, kiongozi wa kambi ya upinzani pamoja na Benny Gantz, Mzayuni mwingine aliyejitoa kwenye serikali ya vita ya Netanyahu walishiriki kwenye maandamano makubwa ya siku ya Jumamosi na kutaka kupinduliwa serikali ya hivi sasa ya utawala wa Kizayuni. Katika maandamano hayo, Lapid alisema kuwa, mazungumzo kati ya vyama tofauti kikiwemo cha Likud yanaendelea kuhusu kupinduliwa serikali ya Netanyahu. Maandamano makubwa yameongezeka dhidi ya Netanyahu kutokana na serikali yake kushindwa kuwakomboa mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa makundi ya muqawama wa Ukanda wa Ghaza huku familia za mateka hao zikiingia barabarani kila siku kumlaani Netanyahu na kundi lake. Familia hizo zinasema kuwa, Netanyahu anajifikiria yeye tu na hajali roho za watoto wa familia hizo. Mara kwa mara familia hizo zimekuwa zikitoa matamko zikisema kuwa, tunawataka Waisraeli wote wamiminike mitaani kumlazimisha Netanyahu afikie makubaliano na makundi ya muqawama ya Palestina ili mateka hao wa Kizayuni waweze kuachiliwa huru.
Vile vile waandamanaji Wazayuni wamekuwa wakiwataka makamanda na majenerali wa kijeshi wa Israel kumzuia Netanyahu asiendelee na siasa zake zilizofeli bali afikie makubaliano ya kukomeshwa vita vya Ghaza na kuachiliwa huru mateka.
Familia za mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa wanamuqawama wa Palestina wanasema kuwa, Benjamin Netanyahu amepata fursa nyingi za kufikia makubaliano ya kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni lakini amekataa bali amekuwa akivuruga fursa hizo. Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kanali ya 12 ya Televisheni ya Israel unaonesha kuwa, karibu thuluthi mbili nzima za Waisraeli wanaamini kuwa wakati umefika kwa Netanyahu kufutwa kikamilifu kwenye ulimwengu wa siasa. Karibu asilimia 85 ya walioshiriki kwenye uchunguzi huo wametaka kuundwe tume na kamati maalumu ya kuchunguza kwa nini akina Netanyahu walishindwa kuzuia operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa iliyoongozwa na HAMAS tarehe 7 Oktoba 2023 na kwa nini miezi 9 sasa jeshi la Israel linafanya mashambulizi makubwa mno lakini limeshindwa kufikia lengo hata moja huko Ghaza.
Si hayo tu, lakini pia familia hizo za mateka wa Kizayuni zinamlaani Netanyahu kwa kufanya mashambulizi ambayo yanapelekea kuangamizwa mateka hao na hajali roho zao. Hii ni kusema kuwa idadi kubwa ya mateka wa Kizayuni waliokuweko mikononi mwa wanamuqawama wa Ghaza wameangamizwa na mashambulio ya kipunguani na kiwendawazimu ya angani na ardhini, ya mizinga, vifaru na makombora yanayofanywa na jeshi kalili la Israel katika ukanda huo. Baadhi ya mateka hao wameachiliwa huru kutokana na hisia za kibinadamu za wanamuqawama wa Palestina na wengine wameachiliwa huru kupitia kubadilisha mateka.
Familia za mateka hao zinalalamika na kumlaani vikali Netanyahu na kundi lake lenye misimamo mikali kupindukia ya Kizayuni, na zinasema mara kwa mara kwamba kuushambulia mji wa Rafah wa kusini mwa Ukanda wa Ghaza kuna maana ya kutekeleza adhabu ya kifo kwa watu wa familia zao ambao ni mateka mikononi mwa harakati za Palestina kama vile HAMAS.
Amma hatua nyingine ya kiwendawazimu ya Netanyahu ni chokochoko zake katika mipaka ya Lebanon. Baada ya kuona kuwa ameshindwa huko Ghaza, sasa waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni anatangaza kuwa anataka kuingia vitani na Hizbullah ya Lebanon. Lakini duru muhimu za Israel zimemuonya na kumwambia wazi kuwa kuingia katika vita vikubwa na Hizbullah kuna maana ya kufutwa Israel katika uso wa dunia. Mambo hayo na mengine mengi, ndiyo yanayozidisha mzozo na mgogoro katika safu za Wazayuni siku baada ya siku.