Jul 02, 2024 12:29 UTC
  • Baraza jipya la mawaziri la Misri kuapishwa Jumatano

Baraza jipya la mawaziri na magavana wa Misri wataapishwa katika Ikulu ya Rais ya Ittihadyiya mjini Cairo kesho Jumatano.

Duru za habari zimearifu kuwa, nyadhifa nyingi za mawaziri na magavana zimekumbwa na mabadiliko katika baraza jipya la mawaziri la serikali ya Rais al Sisi. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya nyadhifa za mawaziri zimeunganishwa na nyingine mpya zikiundwa katika mabadiliko ya baraza jipya la mawaziri la Misri.  Rais wa Misri amechukua hatua hii katika kutekeleza sera zake mpya za kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili nchi hiyo.

Baraza jipya la Mawaziri la Misri litafanya kazi kwa mujibu wa programu zilizoainishwa katika vipaumbele vya taifa ikiwemo kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi, kuendeleza mageuzi ya kimuundo ya kiuchumi na kutilia mkazo uwekezaji. 

Juzi Jumapili Rais Abdel Fattah al Sisi alisisitiza kuwa kipaumbele cha juu zaidi cha baraza jipya la mawaziri ni kupunguza matatizo yanayotokana na kupanda kwa bei na kutayarisha nafasi zaidi za ajira. 

Rais Abdel Fattah al Sisi 

Katika miezi ya karibuni Misri imeathiriwa na uhaba wa fedha za kigeni na kupanda kwa bei za bidhaa duniani masuala ambayo yamezidisha gharama za maisha nchini humo.