Jun 28, 2024 03:14 UTC
  • Ijumaa, 28 Juni, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 21 Mfunguo Tatu Dhulhija 1445 Hijria sawa na Juni 28 mwaka 2024.

Miaka 151 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Dakta Alexis Carrel, mwanabiolojia na mwanafalsafa wa Kifaransa.

Msomi huyo alizaliwa katika mji wa Lyon. Mwaka 1912 Dakta Carrel alitunukiwa tuzo ya heshima ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa katika uwanja wa tiba. Alitumia kipindi fulani katika maisha yake kutalii na kuzitembelea nchi mbalimbali zikiwemo za Kiislamu na kushuhudia kwa karibu mila na tamaduni za nchi hizo. Kwa sababu hiyo Dakta Alexis Carrel amesisitiza mno katika maandishi na vitabu vyake juu ya umuhimu na nafasi ya dini na masuala ya kiroho katika maisha ya mwanadamu.

Dakta Alexis Carrel

Nadharia nyingi za msomi huyo zimo katika kitabu mashuhuri alichokipa jina la "Mwanadamu, Kiumbe Asiyefahamika" ambamo ndani yake anapinga demokrasia ya Kimagharibi.   ***

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Juni 1914 aliuawa Franz Ferdinand, mrithi wa kiti cha ufalme wa Austria akiwa pamoja na mkewe, wakati alipokuwa safarini Sarayevo, mji mkuu wa Bosnia Herzegovina ya leo, baada ya kufyatuliwa risasi na mwanachuo mmoja wa Kiserbia.

Mara baada ya kutokea shambulio hilo, serikali ya Austria ilitaka ipewe nafasi ya kuingilia kati uchunguzi wa faili la kesi hiyo, jambo lililopingwa na serikali ya Serbia.

Baada ya kupita mwezi mmoja tu, Austria ilianza kuishambulia Serbia kwa kisingizio hichohicho, na kuanzia mwezi Agosti mwaka huohuo, vikaanza rasmi Vita vya Kwanza vya Dunia baada ya Ujerumani kuamua kuiunga mkono Austria na ikaishambulia ardhi ya Ubelgiji.   ***

Franz Ferdinand na mkewe

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, yaani tarehe 28 Juni mwaka 1957, Kituo cha Kiislamu mjini Washington, Marekani kilianzisha rasmi shughuli zake.

Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 1949 kwa ushirikiano wa Waislamu wa nchi hiyo na baada ya kuanza kazi hapo mwaka 1957 kiligeuka na kuwa alama yao ya kidini.

Kituo cha Kiislamu cha Washington, mji mkuu wa Marekani kinajumuisha msikiti, shule, maktaba na kadhalika. Ratiba na shughuli mbalimbali za kidini zilizokuwa zikifanyika katika kituo hicho ni miongoni mwa mambo yaliyowafutia sana Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika eneo hilo muhimu.

Shughuli za kituo hicho zilipelekea viongozi wa serikali ya nchi hiyo, kutafuta vijisababu vya kubana kazi zake au kukifunga kabisa.  ****

Kituo cha Kiislamu cha Washington

Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita sawa na tarehe 28 mwezi Juni mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulio makubwa dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake wawili siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Israel ilidai kuwa wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha upekuzi na kuua wanajeshi wake wawili na kumkamata mateka mwingine mmoja. Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji la serikali halali ya Palestina iiliyokuwa ikiongozwa na Hamas walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo makubwa ya jeshi yaliyopewa jina la "Mvua za Kiangazi".

Mbali na hayo, mamia ya raia madhlumu wa Palestina waliuawa shahidi au kujeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya anga na nchi kavu ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.   ***

Na tarehe 8 Tir kwa mwaka wa Kiirani imetambuliwa kuwa ni Siku ya Taifa ya Kupambana na Silaha za Kemikali.

Siku kama ya leo mji wa Sardasht, huko magharibi mwa Iran, ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Wakazi wa mji huo wapatao 110 waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo.

Utawala wa zamani wa Iraq ambao ulikuwa umepoteza matumini ya kushinda vita ulivyovianzisha dhidi ya Iran, ulidhani kwamba kwa kufanya mashambulio ya silaha za kemikali ungeweza kuitwisha Iran matakwa yake kupitia mashambulio hayo ya kinyama, lakini haukufanikiwa kufikia lengo hilo. 

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na silaha za Kemikali na Vijidudu

 

Tags