Oct 22, 2025 12:59 UTC
  • Jumatano, tarehe 22 Oktoba, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 29 Mfunguo Saba Rabiuthani 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 22 Oktoba 2025.

Miaka 774 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Muhammad bin Ahmad Dhahabi, anayejulikana kwa lakabu la Shamsuddin, mpokezi wa Hadithi za Mtume (saw) na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu.

Dhahabi alikuwa akipenda sana kukusanya Hadithi na alifanya safari nyingi katika pembe mbalimbali duniani ili kukamilisha elimu hiyo. Muhammad bin Ahmad Dhahabi alisimuliwa Hadithi nyingi kutoka kwa wazee na maulamaa katika safari zake hizo. Alifuatilia matukio ya historia ya Uislamu na watu mashuhuri ya kuanzia wakati wa kudhihiri Uislamu hadi mwaka 704 na kuandika habari na matukuio ya wataalamu wa Hadithi wa zama hizo.

Matukio hayo aliyakusanya katika kitabu alichokipa jina la Historia ya Uislamu. Vitabu vingine vya msomi huyo ni pamoja na Tabaqatul Qurraa, al Muujamul Saghiir na al Muujamul Kabiir.     

Miaka 119 iliyopita katika siku kama ya leo, Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67.

Alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na fani ya uchoraji tangu akiwa mdogo, lakini kutokana na msisitizo wa baba yake aliingia Chuo Kikuu na kusoma taaluma ya sharia.

Hatimaye akiwa na umri wa miaka 24, baba yake alimruhusu kuendelea na masomo katika taaluma ya uchoraji. Mwanzoni mabango ya uchoraji ya Paul Cezanne hayakupata wafuasi wengi na athari zake za uchoraji zilikabiliwa na ukosoaji mkubwa. 

Mwenendo huo uliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka 50 ambapo hatua kwa hatua alianza kupata umashuhuri kutokana na kuuza mabango yake ya uchoraji.   

Paul Cezanne

Tarehe 30 Mehr miaka 73 iliyopita, Dakta Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Musaddeq, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo alitangaza habari ya kukatwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Uingereza.

Uamuzi huo ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran, baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri.

Dakta Fatimi alisema Tehran imeamua kukata uhusiano na Uingereza kutokana na upuuzaji wa serikali ya London kwa matakwa ya wananchi wa Iran ya kujipatia haki zao, hususan katika uwanja wa kutaifisha sekta ya mafuta. Dakta Fatimi aliwataka viongozi wa London wabadili siasa zao kuhusiana na Iran.   

Dakta Hussein Fatimi

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, aliaga dunia Arnold Joseph Toynbee mwanahistoria mtajika wa Uingereza.

Alizaliwa mwaka 1889. Toynbee alikuwa akifundisha taaluma ya Historia ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha London.

Msomi huyo ameandika vitabu vingi katika uga wa historia na baadhi ya vitabu vyake ni A Study of History, Change and Habit, Choose Life na Civilization on Trial.     

Joseph Toynbee

Miaka 14 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliyekuwa mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudia.

Sultan alikuwa mtoto wa 15 wa kiume wa Mfalme Abdul-Aziz, na mama yake ni Hussa Bint Ahmed Al-Sudairi. Vyombo vya Saudi vilitangaza kuwa, mwanamfalme Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliaga dunia katika mojawapo ya hospitali mjini New York, Marekani. Sultan bin Abdul-Aziz aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 85 baada ya maradhi ya saratani kuenea katika mwili wake wote. 

Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud